Waziri Ummy azindua Kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kwa watumishi wa afya kuhusu ugonjwa wa Uviko - 19
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na wataalam wa afya wanaoendesha kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kuhusu ugonjwa wa Uviko – 19 kwa watumishi wa afya wakati wa uzinduzi wa Kituo hicho uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha mafunzo kwa
njia ya mtandao kuhusu ugonjwa wa Uviko – 19 kwa watumishi wa Afya (Extension
of Community Health and Care Outreach – ECHO) leo katika Hospitali hiyo Jijini
Dar es Salaam.
Baadhi ya wataalam mbalimbali wakifuatilia mafunzo
yaliyokuwa yakitolewa ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya Uviko – 19 wakati
wa uzinduzi wa Kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kuhusu ugonjwa wa Uviko –
19 kwa watumishi wa Afya (Extension of Community Health and Care Outreach –
ECHO) uliofanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Donald Wright, na viongozi mbalimbali baada ya uzinduzi wa wa Kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kuhusu ugonjwa wa Uviko – 19 kwa watumishi wa Afya (Extension of Community Health and Care Outreach – ECHO) uliofanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Khamisi Mussa
*************************************************************************************
Na: Genofeva Matemu
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeipongeza Serikali ya
Marekani kupitia Shirika la Kudhibiti na Kukinga magonjwa la nchini Marekani
(US Centers for Disease Control and Prevention – CDC) kushirikiana na Tanzania
kuboresha huduma za afya na kufungua Kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kwa
watumishi wa afya kuhusu ugonjwa wa Uviko 19 (Extension of Community Health and
Care Outreach – ECHO).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho Waziri wa Afya
Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Kituo hicho kitakua kinatumika kwa ajili ya
kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya nchi nzima kuhusu masuala mbalimbali ya
ugonjwa wa Uviko – 19 ikiwemo jinsi ya kudhibiti maambukizi, namna ya
kumhudumia mgonjwa wa Uviko – 19 na namna ya kufanya vipimo vya ugonjwa huo.
“Tumefungua kituo cha mafunzo kwa njia ya mtandao kwa watumishi
wa afya kuhusu ugonjwa wa Uviko 19 kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani
kupitia shirika la Kudhibiti na kukinga magonjwa la nchini Marekani (US Centers
for Disease Control and Prevention – CDC) pamoja na Taasisi ya Management and
Development for Health – MDH inayofanya kazi na CDC”,
“Kwaniaba ya Serikali tunawashukuru sana shirika la Kudhibiti
na kukinga magonjwa la nchini Marekani (US Centers for Disease Control and
Prevention – CDC) kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha
kuwa tunadhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini Tanzania ikiwemo ugonjwa
wa Uviko – 19”, alisema Mhe. Ummy
Aidha Mhe. Ummy amesema kuwa Shirika la Kudhibiti na Kukinga
magonjwa la nchini Marekani (US Centers for Disease Control and Prevention –
CDC) limekua na utayari katika kusaidia programu mbalimbali za afya hapa nchini
ikiwemo ugonjwa wa HIV, Kifua Kikuu (TB), Malaria, Uviko – 19, chanjo ya Uviko
- 19 pamoja na kuboresha mfumo wa afya nchini.
“Hadi kufika jana Julai 25, 2022 Tanzania tumefanikiwa kutoa
chanjo ya Uviko – 19 kwa watanzania milioni 12.8 ambayo ni sawa na asilimia
41.8 tukiwa ni lengo la kifikia asilimia 70 ya Watanzania wenye umri wa miaka
18 na kuendelea hii ni kutokana na ushirikiano tunaoupata kutoka katika Shirika
hili la CDC”,
“Hadi sasa tuna vituo vikubwa 8 nchini ambavyo vinauwezo wa
kutoa elimu dhidi ya ugonjwa wa Uviko – 19, vituo vidogo vipo 272 na kuna vituo
89 ambavyo wadau mbalimbali wanaendelea kuvifungua yote hii ni kuweza
kukabiliana na ugonjwa wa Uviko – 19”, alisema Waziri Ummy
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu, Utafiti na Ushauri
wa Kitaalam Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Faraja Chiwanga amesema kuwa
kituo hicho ni kikubwa hapa nchini ambacho kitakua kinatoa elimu kwa njia ya
mtandao kwa watumishi wa afya kuhusu ugonjwa wa Uviko 19 lengo ikiwa ni
kuwafikia watumishi wa afya wengi katika maeneo yote nchini hasa maeneo ya
pembezoni mwa nchi.
“Tutahakikisha kuwa watumishi wote wanapata uelewa sahihi wa
jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa Uviko - 19 kama ambavyo tunafahamu yakuwa
ugonjwa huu upo na tutaendelea kukaa nao hivyo kuhakikisha kuwa kiwango kile
kile cha huduma kinachotolewa katika vituo vikubwa kiweze kutolewa hata katika
vituo vidogo vya afya hapa nchini”,
“Ni ngumu kuwa na wataalam mabingwa katika maeneo yote nchini
ndio maana tumeona umuhimu wa kuanzisha mafunzo haya ili wale wataalam mabingwa
watakaokuwa wanafuatilia miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya kupitia mafunzo
haya kwa njia ya mtandao waweze kubadilishana uzoefu na wataalam wenzao”,
alisema Dkt. Faraja
Aidha Dkt. Faraja amewaomba wataalam wa afya walioko katika
vituo vidogo vya afya nchini kujitokeza kuelezea changamoto walizonazo katika
utoaji huduma kwa wagonjwa wa Uviko – 19 ili kupitia programu hiyo waweze
kupatiwa msaada wa jinsi wa kutatua changamoto zao na kuwahudumia wagonjwa hao
kiusahihi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kudhibiti na Kukinga magonjwa
la nchini Marekani (US Centers for Disease Control and Prevention – CDC) Dkt.
Rochelle Walensky amesema kuwa CDC imeshirikiana na Serikali ya Tanzania
kuanzisha mafunzo hayo ili elimu sahihi ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko – 19
iweze kwenda hadi kwa wananchi waliopo maeneo yote nchini hivyo kupunguza
kusambaa kwa ugonjwa huo.
“Wataalamu hawa mabingwa mliowaandaa hapa kwa ajili ya elimu
ya Uviko – 19 na namna ya kujikinga na ugonjwa huu watakua walimu wazuri kwa
wataalam wenzao wa afya waliopo katika vituo vidogo nao kupitia elimu hiyo
wataweza kupeleka utaalam huo kwa wananchi wanaowazunguka hivyo kidhibiti
ugonjwa wa Uviko – 19”, alisema Dkt. Walensky
Comments
Post a Comment