Wauguzi kuweni marafiki wazuri wa ndugu wa wagonjwa mnaowahudumia
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akifunga mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi 13 yamefungwa leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo cha Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya
wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi (Critical Care
Emergence) ambao ni wauguzi kutoka
hospitali mbalimbali nchini wakati wa ufungaji wa kozi hiyo uliofanyika leo
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi (Critical Care Emergence) ambao ni wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini wakati wa ufungaji wa kozi hiyo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akimkabidhi cheti Afisa Uuguzi Scola Riwa baada ya kuhitimu mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliyohudhuliwa na wauguzi 13 yamefungwa leo jijini Dar es Salaam.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah
Kimambo wakati akifunga mafunzo ya wiki 27 ya jinsi wa kuwahudumia wagonjwa wa
dharura na mahututi (Critical Care Emergence) yaliyotolewa kwa wauguzi kutoka
hospitali mbalimbali nchini.
Dkt. Delilah ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi
alisema baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakiona kama ndugu wa wagonjwa ni
wasumbufu lakini hakuna ndugu msumbufu kwani anahitaji kujua maendeleo ya
mgonjwa wake.
“Katika kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kuna uhusiano
wa karibu kati ya mgonjwa, mtoa huduma na ndugu wa mgonjwa wote hawa watatu kuna hali ambayo wanaipata
wakati wa kuuguza. Toeni taarifa ya kila siku ya maendeleo ya mgonjwa kwa ndugu
zake na kuwaambia ukweli kila hatua
anayopitia”,.
“Wagonjwa wengi walioko katika Uangalizi Maalum ICU hawawezi
kula zaidi ya kutumia dawa utakuta ndugu wa mgonjwa anakwenda na chupa iliyojaa
uji akija jioni anaikuta chupa imejaa anabaki kujiuliza mbona hajala na
ikitokea mgonjwa huyo kapoteza maisha ataamini amekufa kwa njaa kitu ambacho
siyo kweli na inakuwa hivyo kwasababu hamtoi taarifa kwa ndugu. Kutoa taarifa
katika hali ya upole ili wawaelewe ni sehemu ya maadili yenu ya kazi kwa
kufanya hivyo mtapunguza malalamiko”, alisema Dkt. Delilah.
Kuhusu kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi Dkt.
Delila alisema kama saikolojia ya mtoa huduma haiko vizuri asiihamishie kwa mgonjwa na siyo
vizuri kufanya hivyo kwani anamtegemea inaweza kuwa anatambua au hatambui kwani
hata wasiokuwa na fahamu wanaelewa kile kinachoendelea.
“Mpe mgonjwa taarifa ya kile unachotaka kukifanya kwake hata kama
hajitambui fahamu kuwa anaelewa kila kinachoendelea hivyo basi kama vile unavyofanya
kwa mgonjwa ambaye anaelewa fanya hivyohivyo na kwa yule ambaye hakuelewi iwe
anasikia au la wewe fanya tu”,alisema Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo.
Aidha Dkt. Delila aliwapongeza wauguzi hao kwa kutenga muda
wao na kwenda kujifunza kozi hiyo na kuwasihi wasiache kusoma na watumie simu
zao za viganjani kusoma masomo ya mtandaoni ya critical care nurses kwani kama
wataacha kusoma watasahau yale waliyojifunza.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt.Peter Kisenge alisema kozi hiyo ilianza
Januari mwaka huu imemalizika salama na wanafunzi wamefaulu vizuri anaamini kwa
jinsi walivyofaulu wataenda kuitumia elimu hiyo kwa kuwasaidia na kuokoa maisha
ya wagonjwa pia watawafundisha wenzao waliowaacha katika Hospitali walizotoka ili nao wapate
elimu hiyo kwani wagonjwa wanaoumwa sana ambao wamelazwa ICU wanahitaji kuishi.
“Mkafanye mabadiliko makubwa katika Hospitali mlizotoka kwani
wauguzi wanaotoa huduma za ICU kwa wagonjwa wa dharura na mahututi wanakitu
maalum ndani yao cha kuwasaidia wagonjwa wenye hali ngumu ambao wanaweza
kupoteza maisha yao wakati wowote lakini
kupitia Mwenyezi Mungu wao wanaweza kuokoa maisha ya wagonjwa hao kitu ambacho
watu wengine hawana”,.
“Ninaipongeza Serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuwasomesha
wataalamu, kujenga majengo ya kisasa zikiwemo ICU na kununua vifaa tiba vya
kisasa. Wafanyakazi hao wanafanya kazi katika ICU na ndiyo waliowafundisha
nyinyi kwani bila kuwepo kwa wataalamu hao msingeweza kupata mafunzo”, alisema
Dkt. Kisenge.
Naye mratibu wa kozi hiyo ambaye ni Afisa uuguzi na mtaalamu
wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi
Joshua Ogutu alisema washiriki wa kozi hiyo ambao walikuwa 13
wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa
aliyepo katika mashine ya kumsaidia kupumua (Ventilator)na jinsi ya kutumia
mashine hiyo.
Jinsi ya kutumia mashine ya Cardiac Monitor ambayo inafanya
uangalizi wa karibu kwa wagonjwa mahututi na kuushtua moyo ulioacha kufanya
kazi (Defibrillation).
Pia walijifunza matumizi ya mashine inayosafisha damu ya
mgonjwa wa figo na jinsi ya kumuhudumia mgonjwa anayehitaji huduma ya
dharura, jinsi ya kutoa tiba maalum za
wagonjwa wa figo, kutoa dawa za wagonjwa wa moyo na jinsi ya kumuhudumia
mgonjwa ambaye moyo wake haufanyi kazi vizuri (Basic Life Support – BLS,
Advanced Cardiac Life Support – ACLS).
Afisa Uuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando
Archileus Dominick ambaye ni mshiriki wa kozi hiyo alisema mafunzo yalikuwa
mazuri na wamejifunza vitu ambavyo
walitarajia kujifunza na vingine ambavyo hawakutarajia kujifunza katika utoaji
wa huduma kwa wagonjwa mahututi na dharura na anaamini kozi hiyo itamsaidia
kutoa huduma bora kwa wagonjwa hao kwani hapo awali alishindwa kuwahudumia
ipasavyo kwakuwa hakuwa na ujuzi wa kutosha.
Epifania Mlay ambaye ni Afisa Uuguzi kutoka Hospitali ya
Rabininsia iliyopo jijini Dar es Salaam aliyeshiriki kozi hiyo alisema jinsi alivyokuwa
kabla hajahudhulia mafunzo hayo ni tofauti na alivyokuwa sasa kwani
amefundishwa vitu vingi ambavyo hakuwa anavijua lakini alikuwa anaviona vikitokea
Hospitalini aliwasihi wauguzi wenzake kuomba kozi hiyo pindi itakapotangazwa kwani
itawaongezea uwezo binafsi wa kufanya kazi.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianzisha kozi hiyo ya wiki 27 ambayo inafanyika mara mbili kwa mwaka lengo likiwa ni kuhakikisha wauguzi ambao ndiyo wanakaa na wagonjwa muda mrefu wodini wanapata elimu ya kutosha ya jinsi ya kuwahudumia wagojwa wa dharura na mahututi ambayo itasaidia kupunguza vifo vinavyotokea ICU.
Comments
Post a Comment