Dkt. Ndugulile: JKCI wajengeeni uwezo madaktari wa hospitali zisizo za rufaa


Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wa Hospitali ya Wilaya Kigamboni wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanyika katika  Hospitali ya Kigamboni.


Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya Kigamboni kwaajili ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo huduma iliyokuwa inatolewa na  wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwajengea uwezo madaktari  wa hospitali zisizo za rufaa ili nao waweze kutibu magonjwa ya shinikizo la damu na kisukari kwa kufanya hivyo kutaipunguzia mzigo taasisi hiyo ya kutibu magonjwa hayo.

Rai hiyo imetolewa jana na Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalaumu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya Kigamboni.

Dkt. Ndugulile alisema utengenezwe utaratibu ambao mgonjwa atakayegundulika  kuwa na tatizo la kisukari au shinikizo la damu kutokwenda moja kwa moja JKCI bali akachukuwa dawa za kutumia katika ngazi ya wilaya au kituo cha afya, akawa anakwenda JKCI baada ya miezi miwili au mitatu kulingana na ushauri wa daktari wake kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza mzigo kwa JKCI na wagonjwa pia.

“Utaratibu huu pia utawajengea uwezo madaktari wa hospitali zisizo za rufaa wa kuweza kubaini na kutibu magonjwa yasiyoambukiza kwa kiwango ambacho wataalamu wanaweza na katika magonjwa ambayo yameshindikana watatoa rufaa kwa wagonjwa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile aliipongeza JKCI kwa kuanzisha mobile kliniki na kusema kuwa ni utaratibu mzuri na wamejitahidi kwenda mbali zaidi na kuwafikia wananchi wengi walioko maeneo ya vijijini ambao kutokana na mazingira yao ni vigumu kufikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa.

“Nimepata faraja kuona kambi hii ya matibabu ya moyo imewafikia watu wengi zaidi wakiwemo wa nje ya wilaya ya Kigamboni, upimaji umewashirikisha wataalamu wa JKCI na wa Hospitali ya Wilaya Kigamboni ambao wamebadilishana ujuzi wa kazi”, alisema Dkt. Ndugulile.

Mbunge huyo wa wilaya ya Kigamboni alisema magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kuongezeka nao wabunge wanaendelea  kuishauri Serikali kuendelea kuweka mifumo ya kuhakikisha magonjwa hayo yanapewa  kipaumbele.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari