Dkt. Timbuka awahimiza Siha kupima magonjwa ya moyo

Mkuu wa Wilaya ya Siha Dkt. Christopher Timbuka akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na waratibu wa Siha Marathon waliofika ofisini kwake kwaajili ya kujitambulisha. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya ya Siha wanafanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya wilaya ya Siha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Dkt. Haji Mnasi akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na waratibu wa Siha Marathon waliofika ofisini kwake kwaajili ya kujitambulisha. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya ya Siha wanafanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano  katika  Hospitali ya wilaya ya Siha.

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi waliofika katika Hospitali ya wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************

Mkuu wa Wilaya ya Siha Dkt. Christopher Timbuka amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Huduma hizo za kibingwa zinatolewa katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya ya Siha.

Dkt. Timbuka alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) waliofika ofisini kwake kwaajili ya kujitambulisha.

“Ni muhimu wananchi wakatumia fursa hii kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo ili kama watakutwa na matatizo waweze kupata matibabu kwa wakati kuliko kusubiri changamoto za ugonjwa kujitokeza kwani gharama za matibabu haya ni kubwa”,.

“Huduma hizi za kibingwa za magonjwa ya moyo zimesogezwa karibu na wananchi  kwa lengo la kuwapunguzia gharama ya kuzifuata katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliyopo jijini Dar es Salaam ni muhimu wananchi wakatumia nafasi hii kupima”, alisisitiza Dkt. Timbuka.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliishukuru JKCI kwa kuwatuma madaktari bingwa pamoja na wataalamu wa lishe ambao wanatoa huduma kwa wananchi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali ya wilaya ya Siha.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda aliushukuru uongozi wa wilaya ya  Siha kwa kuwakea na kukubali kushirikiana na hospitali ya wilaya hiyo katika  kutoa huduma  za matibabu kwa wananchi.

Anna alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kuwepo kwa huduma hiyo kumesaidia wananchi wengi hasa wa mikoa ya pembezoni kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

“Taasisi yetu inaunga mkono jitihada za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa zikiwemo za moyo kwa  wananchi ndiyo maana tumekuja wilayani Siha kuwafuata wananchi ili wapate huduma hii na kwa wale watakaokutwa  na matatizo yanayohitaji matibabu ya kipingwa watapewa  rufaa ya moja kwa moja ya kuja kutibiwa JKCI”.

“Asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowaona katika Taasisi yetu tunawakuta mioyo yao tayari imechoka hii ni kutokana na kuchelewa kupata huduma ya uchunguzi  na matibabu ya moyo,  kwa kuwafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma hii ya tiba mkoba kumesaidia wananchi wengi wanapata huduma za matibabu kwa wakati”, alisema Anna.

Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa licha ya kuwapunguzia gharama ya safari ya kuifuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam pia wamefahamu afya ya mioyo yao ikoje.

“Nimepata elimu ya matumizi sahihi ya dawa za presha nilikuwa sijui kama dawa hizi nitazitumia katika maisha yangu yote kwani mimi ninatatizo la presha na baada ya presha yangu kukaa sawa niliacha kutumia dawa, baada ya kupata elimu hii nitaendelea kutumia dawa sintaacha tena”, alisema Neema Tenga mkazi wa Same.

“Ninashukuru huduma niliyoipata ni nzuri mimi ni mara yangu ya kwanza kupima moyo niliposikia tangazo la huduma hii niliamua kuja kupima. Ninawaomba wananchi wenzangu zinapotokea fursa kama hizi tuzichangamkie mje kupima ili mjue kama mnamatatizo ya moyo au la”,  alishukuru Isah Lipongo  mkazi wa Siha.

Huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya moyo  zinatolewa bila malipo yoyote yale ambapo wananchi wanapimwa kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, uwiano baina ya   urefu na uzito , kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) na mfumo wa umeme wa moyo (ECG).

 


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)