WANANCHI 761 WAPATA HUDUMA YA TIBA MKOBA YA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kumalizika kwa mbio za Siha Marathon 2023 zilizofanyika hivi karibuni mkoani Kilimanjaro.

Wananchi wa Siha wakijadili mambo mbalimbali huku wakisubiri kufanyiwa vipimo vya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku sita ya upimaji na matibabu ya moyo iliyomalizika hivi karibuni katika hospitali ya Wilaya ya Siha.

Na: JKCI

**********************************************************************************************

Watu 761 wamepata huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya Siha. Kambi hiyo ilifanyika kwa muda wa siku sita kuanzia tarehe 18 hadi 23/12/2023 ambapo watu wazima na  watoto walipata huduma ya matibabu.

Kwa upande wa watu wazima waliofanyiwa upimaji wengi wao walikutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na shida za valvu za moyo.

Watoto 55 walifanyiwa uchunguzi ambapo wengine walikutwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu, valvu za moyo kuwa na shida na kutanuka kwa kuta za moyo kupita kiasi.

Wagonjwa wengine kwa mara ya kwanza wamegundulika kuwa na matatizo ya moyo ikiwa ni pamoja na valvu za moyo, kutanuka na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ambapo wagonjwa 66 tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa vipimo zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu.

Katika kambi hii wananchi walipimwa vipimo mbalimbali vya moyo ikiwa ni pamoja na urefu, uzito, kiwango cha sukari mwilini, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) na kipimo cha mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography) pamoja na vipimo vya damu (utendaji kazi wa figo, ini na kiwango cha mafuta kwenye damu).

Tulikuwa na wataalamu wa lishe ambao walitoa elimu ya lishe bora ambayo iliwapa wananchi uelewa wa  kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaweza  kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Katika kambi hii ya matibabu tumewajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali ya wilaya ya Siha ya jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo.

Tunawaomba wananchi muepuke tabia hatarishi zinazoweza kuharibu mioyo yenu hii ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri. Zingatieni  mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora.

 

“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.

Imetolewa na:


Anna Nkinda

Mkuu kwa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano

27/12/2023

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari