Dkt. Mollel: Wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt. Christopher Timbuka funguo za gari moja kati ya matatu yaliyotolewa na Serikali kwa wilaya hiyo ambalo litatumika katika huduma za afya. Licha ya kukabidhi gari hilo Mhe. Dkt. Mollel alifungua kambi maalumu ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya wilaya ya Siha.
Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikweye (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akitoa elimu ya matumizi sahihi ya
dawa za shinikizo la juu la damu kwa mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya ya Siha
kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo
zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Hospitali
hiyo.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 6.7
kwaajili ya kuboresha huduma za afya hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu
ndani na nje ya nchi ili wananchi wengi waweze kupata matibabu ya kibingwa ya
magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin
Mollel wakati akiongea na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha
kwaajili ya kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo
zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.
Mhe. Dkt. Mollel ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha
alisema katika kambi hiyo kwa muda wa siku tatu wataalamu wameona watu 307 kati
yao 37 wamekutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa
rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Kama hawa watu waliogundulika kuwa na matatizo wasingeonwa
katika kambi hii si ajabu wasingeweza kuishi muda mrefu lakini uwepo wa
matibabu haya umewasaidia kugundulika kuwa na mamtatizo ambayo yanahitaji
matibabu ya kibingwa na watapata matibabu mapema”, alisema Mhe. Dkt. Mollel.
“Huduma za matibabu zinazopatikana katika upimaji huu
zinatolewa bila malipo yoyote yale kwani Serikali imegharamia kila kitu na
kutokana na uhitaji kuwa mkubwa JKCI wameongeza siku mbili hivyo basi kambi hii
itamalizika siku ya Jumapili, ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kuja
kupima afya zenu”, alisisistiza Mhe. Dkt. Mollel.
Mhe. Dkt. Mollel alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuboresha huduma za afya na hivyo kuwafanya watanzania na ambao siyo
watanzania kuwa na uhakika wa kupata matibabu ya kibingwa na ndiyo maana Tanzania
inapokea wagonjwa kutoka nchi za jirani ambao wanakuja kutibiwa hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa
JKCI Dkt. Delilah Kimambo alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma ya tiba
mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ya
kuwafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya
moyo.
Pia katika tiba mkoba wanatoa nafasi kwa wale wanaokutwa na
matatizo ya moyo kupata nafasi ya kutibiwa mapema kwa kupewa rufaa na kuwajengea
uwezo wataalamu wa hospitali husika ili baada ya kumalizika kwa kambi ya
matibabu nao waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.
Dkt. Delilah ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kwa
muda wa siku tatu tangu kuanza kwa kambi hiyo ya matibabu wameona watu 307 na
kuna ambao wamekutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu. Valvu, mishipa ya
damu ya moyo kuziba na kwa upande wa watoto walikutwa na matundu kwenye moyo.
“Siku ya Jumapili tutakuwepo katika mbio za Siha Marathon kwaajili
ya kufanya upimaji ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mbio
hizi licha ya kushiriki mbio pia mpime afya zenu, mkimbie kwa afya na mlinde
mioyo yenu”, alisisitiza Dkt. Delilah.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Siha
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mhe. Duncan Urassa aliishukuru Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufika wilayani humo na kutoa huduma kwa
wananchi.
“Watu wengi wamejitokeza kupima afya zao zoezi hili linatija kwani
wananchi wamepewa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia kupambana na magonjwa
yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo pamoja na kubadilisha mtindo wao wa
maisha”.
“Kuna ambao hawakuwa wanajijua kuwa na magonjwa ya moyo baada
ya upimaji wamegundulika kuwa wagonjwa, ninaamini baada ya zoezi hili watu
watabadili mtindo wa maisha na kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara
pamoja na kufanya mazoezi”, alisema Mhe. Urassa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilala ya Siha
Dkt. Haji Mnasi aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kuwajengea uwezo wataalamu
wa Hospitali ya Wilaya ya Siha wa jinsi ya kufanya vipimo vya moyo na kuwatambua wagonjwa wa moyo jambo ambalo
litasababisha wagonjwa wa aina hiyo kutambuliwa na kupata matibabu kwa wakati.
“Leo hii pia tumekabidhiwa gari na vifaa tiba vyenye thamani
ya zaidi ya shilingi milioni 900 ninaishukuru Serikali kwa kujali afya za
wananchi wa Siha kwa niaba ya watumishi wenzangu ninaahidi kuvitunza vifaa hivi
ili viweze kutumika muda mrefu zaidi” alishukuru Dkt. Mnasi.
Uzinduzi huo ulikwenda sambamba na makabidhiano ya gari moja kati ya matatu yaliyotolewa na Serikali kwa wilaya hiyo ambalo litatumika katika huduma za afya na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900 ambavyo vitatumika katika Hospitali ya wilaya ya Siha.
Comments
Post a Comment