SATF warudisha tabasamu la watoto wenye matatizo ya moyo

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Shirika la Social Action Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa mfano wa hundi ya shilingi milioni 60 fedha mbazo zimetolewa jana  kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimshukuru Meneja wa Mradi wa Shirika la Social Action Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa baada ya shirika hilo kutoa msaada wa shilingi milioni 60 fedha mbazo zimetolewa jana kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 10.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza jana mara baada ya kupokea msaada wa shilingi milioni 60 kutoka kwa Shirika la Social Action Fund (SATF) fedha mbazo zimetolewa kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 10.

Meneja wa Mradi wa Shirika la Social Action Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa akizungumza jana mara baada ya kutoa msaada wa shilingi milioni 60 fedha mbazo zimetolewa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 10 wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************

Shirika la Social Action Trust Fund (SATF) limetoa msaada wa shilingi milioni 60 fedha ambazo zitatumika kwaajili ya kulipia gharama ya upasuaji wa moyo kwa watoto 10 wanaotibiwa  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akipokea msaada huo jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alilishukuru shirika hilo kwa msaada walioutoa na kusema kuwa umeokoa maisha ya watoto ambao siku za baadaye wanaweza kuwa viongozi wakubwa katika nchi.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema watoto wengi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wanatoka katika familia zenye kipato cha chini na kuna ambao wanashindwa kabisa kulipia gharama za matibabu.

“Tunawashukuru SATF kwa kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha watanzania wanapata huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo, hawa watoto mliowasaidia leo mmeweza kurudisha tabasamu lao kwani baada ya matibabu watapona na kuendelea na maisha kama watoto wengine”.

“Gharama za upasuaji wa moyo ni kubwa na kuna ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 10, kutokana na gharama hizi tumekuwa tukiwahimiza wananchi kujiunga na bima za afya ambazo zitawasadia kulipia gharama za matibabu kipindi watakapoumwa”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka Shirika la Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa alisema shirika hilo limetimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na katika kusherehekea wameona watoe fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 60 kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto.

“Katika kuadhimisha miaka 25 tuliona tuwasaidie watoto wenye matatizo ya moyo kwani tunaona gharama zao za matibabu ni kubwa sana na kama familia haina uwezo wa kulipia inakuwa ni changamoto kwao”.

“Shirika letu linajihusisha na kusaidia jamii katika afya, elimu, ulinzi na usalama wa mtoto na uwezeshaji kiuchumi katika ngazi ya kaya huduma hizi tunazitoa katika mikoa 19 na tumeshazifikia wilaya 36”, alisema Rutabanzibwa.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa watoto waliopata msaada huo Elizabeth Bwenda alilishukuru shirika hilo na kusema kuwa msaada huo utawasaidia watoto wao kupata matibabu na kuwasihi wazazi ambao watoto wao wanamatatizo ya moyo na hawana uwezo wa kulipia gharama wasikate tamaa kwani Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanalipia gharama hizo.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari