Balozi Polepole kushirikiana na JKCI kuboresha matibabu ya moyo
Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey
Polepole akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo jijini Dar es
Salaam kwaajili ya kuona namna ambavyo watashirikiana katika kuboresha huduma
ya matibabu ya moyo.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Mhe. Balozi Polepole ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea
Taasisi hiyo kwaajili ya kuona namna ambavyo nchi ya Cuba inaweza kushirikiana
na Tanzania katika utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo.
Alisema nchi ya Cuba imepiga hatua kubwa katika sekya ya afya na kuna madaktari wengi wa Tanzania wamesoma
nchini humo, ataangalia namna ambavyo
madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini Cuba watashirikiana na madaktari bingwa
wa JKCI katika kutoa huduma ya tiba bobezi kwa wananchi.
“Nchi ya Cuba ina
viwanda vingi vinavyotengeneza vifaa tiba mbalimbali vikiwemo vya moyo kwa bei
naafuu ukilinganisha na soko la dunia, nitaangalia namna ya kuwaunganisha na
viwanda hivi ili muweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia wananchi”,
alisema Mhe. Balozi Polepole.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alimshukuru Balozi Polepole kwa kuitembelea
Taasisi hiyo na kusema kuwa wataendelea kushirikiana naye katika kuboresha
huduma za afya ya moyo kwa watanzania.
“Taasisi yetu imekuwa na ushirikiano mzuri na Mhe. Balozi
Polepole kwani wakati yuko nchini Malawi alifanikisha kujenga mahusiano
yaliyowezesha wataalamu wetu kwenda nchini humo kutoa huduma za matibabu ya
moyo kwa wananchi. Hivi sasa tunapokea wagonjwa wengi kutoka nchini Malawi
ambao wanakuja kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.
“Ninaamini kuwepo kwake nchini Cuba Taasisi yetu itafaidika
kwa wataalamu wetu kujengewa uwezo zaidi na kupata vifaa tiba vya matibabu ya
moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Comments
Post a Comment