JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina akikata utepe wakati wa
kuzindua magari mawili yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwaajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa
JKCI. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya uzinduzi wa magari mawili yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwaajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia magari mawili ambayo yatatumika kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Shukurani hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina wakati akizundua
magari hayo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Asha ambaye pia ni mratibu wa huduma za afya ya uzazi na
mtoto mkoa wa Rukwa alisema magari hayo yametolewa ili kusaidia katika huduma
za afya ambapo katika Taasisi hiyo yatasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo
watakaohitaji huduma ya gari la wagonjwa.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya Wadhamini alisema Mhe. Dkt. Samia ametoa magari zaidi ya 700
katika Hospitali zote nchini kwaajili ya kutoa huduma katika hospitali ambapo
JKCI imepokea magari mawili.
“JKCI tumepata magari mawili, moja likiwa gari la kuhudumia
wagonjwa (Ambulance) na lingine kwaajili ya kusimamia usimamizi shirikishi
unaofanywa na wataalamu wabobezi wa magonjwa ya moyo waliopo JKCI”, alisema
Asha.
Asha alisema gari la kuhudumia wagonjwa litasaidia katika
kazi za kuchukua wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Dar es
Salaam pale litakapohitajika.
“Lengo kubwa la kupewa gari la kuhudumia wagonjwa ni
kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati kwani mara nyingi kumekuwa na
tatizo la baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitali kwaajili ya kupata
huduma pale wanapokuwa na dharura”, alisema Asha.
Aidha Asha ametoa maelekezo ya kuitaka JKCI kuwa na namba ya
dharura ambayo itawaruhusu wananchi kupiga simu wakati wowote wanapohitaji
msaada wa gari linalohudumia wagonjwa.
“Sasa hivi Taasisi yetu inahudumia wagonjwa wengi waliopo
ndani ya nchi na wengine kutoka nchi za jirani, hivyo kupitia gari hili
tunaenda kurahisisha huduma za kupokea wagonjwa wanapofika katika uwanja wetu
wa ndege wanapokelewa na kufikishwa JKCI kwa haraka”, alisema Asha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali wananchi wake
ndio maana ikaona umuhimu wa kutoa magari hayo ili kurahishisha huduma
zinazotolewa na JKCI.
Dkt. Kisenge alisema JKCI imefarijika kupokea magari hayo
kwani sasa hivi imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka mikoa
mbalimbali na nje ya nchi wengi wao wakiwa na hali isiyoridhishwa hivyo kwa
kutumia magari hayo wagonjwa watapokelewa kirahisi.
“JKCI inapokea wagonjwa kutoka nchi zaidi ya 20 wengi wao wanapofika katika uwanja wetu wa ndege wanahitaji gari la kuhudumia wagonjwa kuwapokea na kuwafikisha hapa kwetu; ndani ya miezi mitatu tumeweza kupokea wagonjwa takribani 100 kutoka nje ya nchi”, alisema Dkt. Kisenge.
Comments
Post a Comment