Tanzania, China zasaini mkataba wa ujenzi wa hospitali mpya ya JKCI Mloganzila

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Balozi wa Jamhuri wa Watu wa China Mhe. Chen Mingjian wakionesha mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mkataba huo umesainiwa leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Balozi wa Jamhuri wa Watu wa China Mhe. Chen Mingjian wakisaini mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mkataba huo umesainiwa leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Chen Mingjian, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wafanyakazi na wataalamu wa afya kutoka Tanzania na china wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Picha Na

********************************************************************************************************************

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Jamhuri ya Watu wa China zimesaini Mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa hospitali mpya ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itakayojengwa Mloganzila.

Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam pamoja na kufanya makabidhiano ya vifaa tiba na dawa kutoka kwa timu ya madaktari wa Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni ushahidi rasmi kwamba mradi huo umeingia katika hatua mpya ya utekelezaji  na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China unavyoendelea kuzaa matokeo yanayogusa moja kwa moja maisha na ustawi wa watanzania.

“Upande wa sekta ya afya sisi tumekuwa wanufaika wakubwa sana wa ushirikiano na Jamhiri ya Watu wa China. Moja ya matokeo yake ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo hapo nyuma hatukuwa nayo. Taasisi hii tuliipata kutokana na ushirikiano ambao tumekuwa nao”, alisema Dkt. Magembe

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian alisema China imekuwa mshirika wa Tanzania katika sekta ya afya kwa muda mrefu akitolea mfano JKCI ambayo ilikabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania Septemba 2012 baada ya kujengwa kwa msaada wa China.

“Ninafurahi kuona kwamba baada ya zaidi ya muongo mmoja wa maendeleo taasisi inaendelea kufanya vizuri. Wagonjwa wengi wa Tanzania hawalazimiki tena kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya upasuaji wa moyo bali wanaweza kupata huduma bora za matibabu hapa nchini kwa wakati”, alisema Mingjian

 

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema ujenzi wa hospitali mpya ya JKCI utaunga mkono mipango ya JKCI kuongeza huduma za kibingwa ikiwemo mpango wa kuanza kutoa huduma za upandikizaji wa moyo (heart transplant) ifikapo mwaka 2030.

“Mradi huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri unaofanywa na Tanzania na China ambao ulianza tangu miaka ya sitini. Hospitali itakayojengwa itakuwa na teknolojia ya hali ya juu na itaifanya JKCI kuwa kituo kikubwa cha matibabu na upasuaji wa moyo kwa Afrika Mashariki na Kati”, alisema Dkt. Kisenge.

Ujenzi wa Hospitali mpya ya moyo nchini unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma bingwa na za kisasa za uchunguzi na matibabu ya moyo pamoja na kuimarisha utaalamu, teknolojia na miundombinu ya huduma za moyo nchini.








Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma