Mabondia wa ngumi za kulipwa wahimiza upimaji wa afya kwa wanamichezo
Fundi Sanifu wa Moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Nachai Mfinanga akimpima
mfumo wa umeme wa moyo mchezaji wa ngumi za kulipwa Tanzania aliyefika
kufanyiwa uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya siku tatu ya upimaji wa
magonjwa ya moyo kwa wanamichezo hao inayofanyika katika viwanja vya Mafia
boxing Sports Promotion Magomeni jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Florence Silayo akimpima
shinikizo la damu mchezaji wa ngumi za kulipwa Tanzania wakati wa kambi maalumu
ya siku tatu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo hao inayofanyika
katika viwanja vya Mafia boxing Sports Promotion Magomeni jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
**********************************************************************************************************************
Makocha na mabondia wa ngumi za
kulipwa nchini wametaka uchunguzi wa afya kupewa kipaumbele kwa wanamichezo hao
ili kubaini mapema magonjwa yanayoweza kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati
wa kambi maalumu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa ngumi za
kulipwa Tanzania inayofanyika katika viwanja vya Mafia Boxing Sports Promotion
vilivyopo Magomeni jijini Dar es Salaam wamesema huduma hizo ni muhimu katika
kuwasaidia mabondia kufahamu hali za afya zao.
Bondia wa zamani wa ngumi za
kulipwa nchini Said Yazidu alisema uchunguzi wa afya ni muhimu kwa mabondia kwa
sababu kufanya mazoezi mara kwa mara hakumaanishi kuwa wanamichezo hawana
changamoto za kiafya.
“Ni jambo zuri sana kwa wachezaji
kufahamu afya zao kwa sababu mchezaji anaweza kufanya mazoezi kila siku kumbe
ana matatizo ya kiafya ambayo hayajui, naomba zoezi hili lisiwe la muda tu bali
liwe endelevu na ikiwezekana lifikishwe katika mikoa mingine ili mabondia wote
wapimwe moyo”, alisema Yazidu.
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini
Frank Shagembe aliwahimiza mabondia ambao hawajapata nafasi ya kupima afya zao
kujitokeza kwa wingi wanapopata fursa hiyo akieleza kuwa uchunguzi wa afya
unaweza kusaidia kubaini matatizo ambayo hayawezi kutambuliwa kwa kutegemea
hali ya mwili pekee.
Kwa upande wake kocha na refa wa
ngumi za kulipwa Tanzania Kondo Nassoro alisema amefurahishwa na mwitikio wa
mabondia waliojitokeza kufanya uchunguzi wa afya na kuwasisitiza mabondia umuhimu wa kupima afya zao kabla ya kushiriki
katika mchezo huo unaohitaji maandalizi na uangalizi wa karibu wa kiafya.
“Ni muhimu kabla mabondia
hawajaingia ulingoni kupima vipimo vya moyo, wamekuwa wakishiriki katika
michezo bila kupima afya zao hivo JKCI imetupa elimu ambayo tutaifanyia kazi
kuwalinda wanamichezo wetu”, alisema Nassoro.

.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment