Milioni 100 zatolewa matibabu ya moyo kwa watoto


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge hundi ya shilingi milioni 100 iliyotolewa leo katika Viwanja vya Farasi Oyster bay jijini Dar es Salaam na Benki ya CRDB fedha zilizokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwaongoza viongozi wengine katika matembezi ya kilometa 5 wakati wa mbio za CRDB Marathon kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI na wanawake wenye ujauzito hatarishi wanaotibiwa CCBRT leo jijini Dar es Salaam. 


Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Magreth Ng’ondya na Afisa Uuguzi wa Taasisi hiyo Benson Bisare wakimsikiliza mwananchi aliyeshiriki mbio za CRDB Marathon kabla ya kumpatia huduma wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felister Charles akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyeshiriki mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Oyster bay jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo mara baada ya kupokea hundi ya shilingi milioni 100 fedha zilizokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio za CRDB Marathon msimu wa nne kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI. 


Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakionyesha medali zao baada ya kumalizika kwa mbio za CRDB Marathon msimu wa nne kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo leo katika Viwanja vya Farasi Oyster bay vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Na: JKCI
******************************************************************************************************************************
Shilingi Milioni 100 zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB Marathon msimu wa nne kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay jijini Dar es Salaam Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya zaidi ya asilimia 80 kuchangia gharama za matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.

Dkt. Hussein alisema panapotokea wadau kama benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB Marathon kusaidia sehemu iliyobaki katika ruzuku ya masuala ya afya hupunguza jukumu la serikali ambayo ingelazimika kubeba mzigo wote. 

“Nimefurahi kusikia mbio hizi zinaendelea kuwasaidia watoto wetu kupata huduma za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani imekuwa ikifanya kazi nzuri kutibu watanzania wenye changamoto ya magonjwa ya moyo kutoka pande zote za nchi yetu”, Alisema Dkt. Hussein.

Dkt. Hussein alisema bado zipo familia nyingi ambazo hata asilimia tatu zinazobaki baada ya ruzuku kutolewa na serikali hazina uwezo wa kumudu gharama za matibabu yakiwemo magonjwa ya moyo hivyo kuwaomba wadau kuendelea kutafuta fedha kusaidia watu kupata matibabu hayo.

“Bado mahitaji katika sekta ya afya ni makubwa hivyo ni jambo la faraja kwetu kupata mchango huu wa mbio za CRDB ambao unasaidia kuongeza nguvu kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali”, alisema Dkt. Hussein.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto ambao wanatibiwa katika Taasisi hiyo. 

Dkt. Kisenge alisema Benki ya CRDB kwa miaka minne mfululizo imekuwa sehemu ya kurejesha tabasamu kwa watoto ambao wanatoka katika mazingira magumu hivyo kushindwa kugharamia matibabu lakini kupitia mbio hizo watoto wamekuwa wakipatiwa matibabu.

“Gharama za matibabu ya moyo ni kubwa, hii inatokana na vifaa vinavyotumika kuwa na gharama kubwa, kupitia mbio za CRDB Marathon watoto wanaotoka katika mazingira magumu hupata nafasi ya kutibiwa magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge 
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya CRDB itaendelea kuzifanya mbio za CRDB kuwa endelevu kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa. 

Abdulmajid alisema Mbio za CRDB kwa mwaka 2020 zilichangia fedha kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 100, mwaka 2021 pia walichangia fedha za upasuaji wa moyo kwa watoto 100, na mwaka 2022 zilichangia fedha kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 125. 

“Mwaka huu CRDB Marathon inatoa fedha milioni 100 kwa ajili ya watoto wetu wanaotibiwa JKCI tukiendelea kuwarejeshea tabasamu watoto wenye magonjwa ya moyo ambao wamekuwa wakihitaji msaada kufanikisha matibabu yao”, alisema Abdulmajid
Msimu wa nne wa mbio za CRDB Marathon umelenga kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, kujenga kituo cha afya ya mama na mtoto visiwani Zanzibar, kuchangia matibabu ya akina mama wenye ujauzito hatarishi na changamoto ya Fistula wanaotibiwa CCBRT, pamoja na kuwekeza katika programu ya kuipendezesha Tanzania kwa kuimarisha bustani za Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari