Waishukuru JKCI kwa kuwasogezea huduma za matibabu ya moyo


Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazahura akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi (Echocardiograph – ECHO) mtoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH)


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akizungumza na mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa MRRH

Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga akimsikiliza mwananchi wa mkoa wa Kilimanjaro akijibu maswali ya ufahamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH)

Na: JKCI

**************************************************************************************************************

Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wameishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufikisha huduma za kibingwa za matibabu ya moyo mkoani Kilimanjaro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) wananchi hao wamesema uhitaji wa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo mkoani humo ni mkubwa.

Elishadai Kimaro mkazi wa Kilimanjaro alisema kutokana na wingi wa watu kutoka mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya moyo toka kambi hiyo kuanza imekuwa kubwa hivyo watu kurudishwa nyumbani na kurejea tena siku inayofuata.

“Ninaiomba Serikali huduma za matibabu ya moyo hapa mkoani kwetu zifanyike mara kwa mara au ikiwezekana tuwe na hospitali yetu inayotoa huduma hizi za matibabu ya moyo, kambi maalum ya siku tano na baadaye wataalamu kuondoka haitoshelezi kufikia mahitaji ya wanakilimanjaro”, alisema Kimaro.

Kimaro alisema kupitia kambi hiyo amepata nafasi ya kuchunguza afya ya moyo wake kwani alikuwa na hofu ya kuwa na matatizo ya moyo lakini hakujua ni nini afanye hadi hapo aliposikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete hivyo naye kutumia fursa hiyo kupima.

Twaha Masawe mkazi wa Kilimanjaro alisema huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa afya kutoka JKCI amezipenda kutokana na watoa huduma wanavyozungumza vizuri na wagonjwa na kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Masawe alisema kupitia kambi hiyo ameelimishwa kutokuacha kutumia dawa za shinikizo la damu na kama ataacha anaweza kupata madhara katika moyo wake ama kupata kiharusi.

“Namshukuru Mungu toka nilipogundulika kuwa na shinikizo la damu nimekuwa nikitumia dawa, kupitia elimu niliyoipata hapa nitaendelea kutumia dawa kama inavyotakiwa sitapenda kuona napata madhara mengine ya kiafya yanayoletwa na tatizo la shinikizo la damu”, alisema Masawe

Naye Isha Rashidi Mkazi wa Kilimanjaro alisema ujio wa madaktari bingwa wa moyo Mkoani Kilimanjaro umekuwa fursa kwake kupima moyo wake kutokana na kupenda kwake kuchunguza afya yake lakini pia kuna hali anazozipata mara kwa mara angependa kujua tatizo lake.

Isha alisema baada ya vipimo vya moyo kufanyika yupo tayari kupokea majibu yake na kama atakuwa na shida ya moyo atafuata mtindo bora wa maisha ili kuweza kuepukana na magonjwa ya moyo.

“Kuna wakati napata maumivu kwenye moyo na kusikia mapigo yangu ya moyo kupiga kwa kasi japo sio mara kwa mara inaweza pita hata miezi miwili ndio nikasikia tena hali hii, nipo tayari kujua shida niliyonayo na kufuata ushauri wa madaktari”, alisema Isha

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari