JKCI Dar Group yaboresha huduma ya dharura

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiangalia namna ambavyo wataalamu wa afya wa JKCI Dar Group wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura wakati wa uzinduzi wa Kitengo cha wagonjwa wa dharura katika Hospitali hiyo leo jijini Dar es Salaam


Daktari wa usingizi na mkuu wa timu ya kuratibu jinsi ya kuokoa wagonjwa wa dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Faraji Lydenge akimuonyesha mtaalamu wa afya wa Hospitali ya JKCI Dar Group namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura wakati wa uzinduzi wa kitengo cha wagonjwa wa dharura katika Hospitali hiyo leo jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kitengo cha wagonjwa wa dharura kilichopo Hospitali ya JKCI Dar Group leo jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angella Muhozya akielezea huduma zinazotolewa katika kitengo cha wagonjwa wa dharura wakati wa uzinduzi wa kitengo hicho kilichopo Hospitali ya JKCI Dar Group leo jijini Dar es Salaam

Na: JKCI
*************************************************************************************************************

Huduma za dharura kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo zimeboreshwa kwa kuwekeza vifaa vya kisasa na wataalamu mabingwa wa kutoa huduma hizo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya Dar Group. 

Kitengo hicho cha dharura Hospitali ya JKCI Dar Group sasa kimeimarishwa kwa kuwekeza vifaa vyenye gharama ya shilingi milioni 760 ambavyo ni mashine za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) na mashine za kiwango cha juu za magonjwa ya dharura Advanced Cardiac Monitors, Defibrillator, Emergency Trolley na Ventilator. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema tangu serikali ilivyoipa dhamana JKCI kusimamia Hospitali ya JKCI Dar Group imeendelea kuimarisha huduma na kuongeza vifaa vya kisasa katika kitengo cha magonjwa ya dharura. 

“Tumeimarisha kitengo cha dharura kwa kuwekeza madaktari bingwa wanaotoa huduma kwa wagonjwa mahututi wawili na kutoa mafunzo ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura kwa wataalamu wengine wa afya wanaofanya kazi katika Hospitali hii”, alisema Dkt. Kisenge. 

Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alimshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika uboreshwaji wa Hospitali hiyo kwa kuendelea kuwekeza vifaa vya kisasa hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi. 

“Katika muendelezo wa kusogeza huduma kwa wananchi JKCI inaendelea kupeleka huduma mikoani ambapo hadi sasa tayari tumeshatembelea mikoa 11 na kuona watu zaidi ya 7000 ambao wengi wao hawakuwahi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angella Muhozya alisema tokea kuanzishwa kwa kitengo cha dharura Hospitali ya JKCI Dar Group mwezi Desemba mwaka jana idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka kutoka wagonjwa watatu hadi watano ambapo sasa kitengo kinapokea wagonjwa tisa hadi 15 wanaohitaji huduma za dharura.

“Kutokana na wingi wa wagonjwa tumeona kuna ulazima wa kuongeza vitendea kazi na wataalamu wabobezi ili tunavyokuza huduma pia tuwe na uwezo wa kumudu mahitaji yote yanayohitajika kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura ndio maana Taasisi ikawekeza vyakutosha”, alisema Dkt. Angella

Dkt. Angella alisema huduma ya magonjwa ya dharura hapo awali ilikuwa ikitolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) peke yake lakini baada ya wataalamu wa afya kupata mafunzo ya kutoa huduma hiyo huduma za dharura zinaanza kupatikana na maeneo mengine kama ambavyo sasa inapatikana Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. 

“Kwasasa JKCI kuwa na wataalamu wabobezi wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura ni hatua kubwa kwani wataalamu hao kwa nchi nzima sio zaidi ya 15 hivyo kuifanya taasisi yetu kuwa na viwango vinavyokubalika kimataifa”, alisema Dkt. Angella

 

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari