JKCI kushiriki Kongamano la nane la dunia la wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto nchini Marekani
Na: Stella Gama – Dar es Salaam
Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
watano kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushiriki Kongamano la nane
la dunia la watoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto linalofanyika
nchini Marekani.
Kongamano hilo linatarajiwa kuanza tarehe 28 agosti hadi 3
septemba 2023 ambapo jumla ya washiriki zaidi ya 4500 kutoka nchi mbalimbali
duniani kushiriki.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari bingwa wa moyo
kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naizhijwa Majani alisema
kongamano hilo hufanyika kila baada ya miaka minne ambapo mara ya mwisho
lilifanyika mwaka 2017 Barcelona nchini Spain.
“JKCI iliweza kushiriki katika kongamano la saba
lililofanyika nchini Spain na kujifunza kuhusu msingi wa data shirikishi wa
uboreshaji wa ubora wa huduma kimataifa (International Quality Improvement Collaborative
Data Base - IQIC) inayosaidia kuangalia masuala ya ubora kwenye huduma za
matibabu ya moyo kwa watoto”,
“Baada ya kujifunza tuliweza kuanzisha hapa JKCI data base
hiyo na hadi sasa Tanzania ni kati ya nchi tatu za Afrika inayotumia data base hiyo
inayosimamiwa na wataalam waliopo Boston”, alisema Dkt. Naizhijwa
Dkt. Naizhijwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa
Huduma JKCI alisema kupitia data base hiyo JKCI inapeleka taarifa zote za
upasuaji wa moyo unaofanywa, maendeleo ya wagonjwa, na aina ya upasuaji unaofanywa
na kulinganishwa na wenzao wa Afrika na nchi nyingine nje ya Afrika.
Aidha Dkt. Naizhijwa alisema katika kongamano la nane
wataalam wa JKCI wameweza kutuma majalada 9 ili yaweze kutumika ambapo majalada
7 yamekubaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kongamano hilo.
“Ni nafasi ya kipekee kwetu sisi kwani majalada hadi yaweze
kukubalika kuwasilishwa katika kongamano hili la kipekee kwa watoa huduma za
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto lazima yakidhi viwango vinavyohitajika”,
“Kupitia kongamano hili JKCI inapeleka kazi zake ili ziweze
kuonekana na kuitangaza Taasisi, kutengeneza uhusiano na wataalam kutoka nchi
mbalimbali duniani pamoja na kufungua fursa za masomo, utafiti na kubadilishana
uzoefu”, alisema Dkt. Naizhijwa
Comments
Post a Comment