Zaidi ya wananchi 7000 wafikiwa na huduma ya tiba mkoba


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH.

Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) Anandumi Mmari akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kilalo Barati akimpima shinikizo la damu mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH

 Na: JKCI

**************************************************************************************************************

Wananchi zaidi ya 7000 wafikiwa na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kupitia huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge leo wakati akifungua  kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayoendelea mkoani Kilimanjaro katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH).

Dkt. Kisenge alisema JKCI imekuwa ikifanya huduma ya tiba mkoba katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ambapo hadi sasa mikoa 11 ya Tanzania bara na Zanzibar imeshafikiwa na wananchi takribani 700 kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kambi hiyo ya matibabu ya moyo ni muendelezo wa tiba mkoba ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yenye nia ya kuwafikishia wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro huduma ya tiba bobezi ya magonjwa ya moyo mahali walipo.

“Nia ya JKCI kufanya kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi ni kuhakikisha kuwa tunaendeleza ujuzi kwa wataalamu wa afya wa hapa Mawenzi pamoja na kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wana magonjwa ya moyo”,

“Mwitikio katika Mkoa huu wa Kilimanjaro umekuwa mkubwa sana ndani ya siku mbili tayari wagonjwa 600 wamefika katika Hospitali hii kwa ajili ya kupatiwa huduma, wagonjwa wengi wanaofika tumewakuta na shinikizo la damu na hii inatokea katika kila mkoa tunaoenda ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umekuwa changamoto kwa watu wengi hivyo kupata madhara ya moyo kutanuka”,

Dkt. Kisenge alisema kuwa JKCI Itaendelea kufanya kambi hizo katika mikoa mingine iliyobaki lengo likiwa kuendeleza dhana ya kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi pale walipo.

“Katika kambi hii pia tunatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto ambapo kwa siku hizi mbili watoto waliofanyiwa uchunguzi wengi wao wamekutwa na matundu kwenye moyo”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Dkt. EdnaJoy Munisi aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Dkt. EdnaJoy alisema Mwitikio wa kambi maalum ya matibabu ya moyo umekuwa mkubwa tofauti na ilivyotarajiwa lakini timu ya wataalamu wa afya wa Mawenzi kwa kushirikiana na wenzao waliotoka JKCI wamejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anayefika katika Hospitali ya Mawenzi anapatiwa huduma kwa wakati na kwa ufanisi.

“Tunawasihi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani kuendelea kufika katika Hospitali ya Mawenza kupata fursa ya kupima moyo kwani ni fursa ya pekee hasa kwa watu wazima ambao mara nyingi hushindwa kusafiri kufuata huduma mahali zilipo”, alisema Dkt. EdnaJoy

Naye mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi kwaajili ya kufanya vipimo vya moyo Helen Kavishe alisema furaha ya watu wa Kilimanjaro haieleziki kwa kufikishiwa huduma ya kibingwa ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambayo wengi wao hawakutarajia ingekuwa rahisi hivyo kupata huduma hiyo.

Helen alisema kutokana na wingi wa watu imemchukua siku mbili kupata huduma lakini kutokana na umuhimu wa matibabu ya moyo haikuwa shida kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kurejea tena siku ya pili ili kufanikisha matibabu hayo.

“Tunaomba huduma kama hizi wakati mwingine zipelekwe na maeneo ya vijijini ili wote kwa pamoja tuweze kufaidika na matibabu haya ya kibingwa kwani kiuhalisia tunaona hapa uhitaji ni mkubwa na wagonjwa ni wengi”, alisema Helen

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari