Jengo jipya la JKCI kujengwa Mloganzila


Wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China wakiangalia jiwe la msingi lililowekwa katika jengo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kukutana na uongozi wa JKCI kujadiliana kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo jipya la JKCI mwishoni mwa mwaka huu litakalojengwa eneo la mloganzila.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Tatizo Waane akizungumza wakati wa kikao na wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kujadiliana kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo jipya la JKCI mwishoni mwa mwaka huu litakalojengwa eneo la mloganzila.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Liggyle Vumilia akizungumza wakati wa kikao na wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kujadiliana kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo jipya la JKCI mwishoni mwa mwaka huu litakalojengwa eneo la mloganzila.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Tatizo Waane akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China mara baada ya kumalizika kwa kikao na wajumbe hao kujadiliana kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo jipya la JKCI mwishoni mwa mwaka huu litakalojengwa eneo la mloganzila.

Na: JKCI

*********************************************************************************************************

Jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka 2023 eneo la Mloganzila kupanua huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na kutoa nafasi kwa wananchi wengi kupata huduma kwa wakati.

Jengo hilo linalojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Watu wa China litakuwa jengo la pili linalotoa huduma za matibabu ya moyo kujengwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao kifupi na wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Liggyle Vumilia aliipongeza JKCI kwa kuendeleza mahusiano na nchi ya China tangu pale yaliponzishwa kipindi cha Serikali ya awamu nne. 

Dkt. Vumilia alisema Serikali ya Tanzania imeendeleza mahusiano na Serikali ya Watu wa China ambapo sasa China inaleta watalaamu wa afya Tanzania kushirikiana na madaktari wa Tanzania kutoa huduma za afya, kuwapeleka wataalamu wa afya nchini china kwa ajili ya kupata elimu pamoja na ushirikiano katika kutengeneza miundombinu mizuri ya kutoa huduma za afya.

“Nia kubwa ya ugeni huu ni kuendelea kukuza mahusiano yaliyokuwepo kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, tunaamini ujio wao utasaidia kuendeleza mahusiano yaliyopo na kuhakikisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaendelea kukua kwa kuanzisha ujenzi wa jengo la JKCI eneo la mloganzila”, alisema Dkt. Vumilia

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Tatizo Waane alisema hadi sasa Serikali ya Watu wa China imeshatuma wataalamu wake kutembelea eneo litakapojengwa jengo la JKCI eneo la mloganzila na kufanya upembuzi yakinifu uliosaidia kuainisha mahitaji ya vitu vinavyohitajika kuweza kufanikisha ujenzi uliokusudiwa.

Dkt. Waane alisema kwa sasa JKCI imekuwa sana hivyo Serikali kuona kuna umuhimu wa kupanua huduma kwa kuwa na Jengo lingine la moyo eneo la Mloganzila kuweza kuwafikia watanzania wote wanaohitaji huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.

 “Jengo jipya la JKCI litakalojengwa eneo la Mloganzila litakuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo JKCI ya sasa na kurahisisha huduma za afya kwa wananchi wote”, alisema Dkt. Waane 

Naye Mkuu wa kitengo cha uhakiki ubora wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizhijwa Majani alisema jengo jipya litakalojengwa eneo la mloganzila litaenda kufanana na jengo lililopo sasa la JKCI lakini jengo hilo jipya litakuwa kubwa zaidi kutokana na uhitaji wa watu kutaka huduma za matibabu ya moyo kuongezeka.

“Tunategemea jengo jipya la JKCI litakalojengwa eneo la mloganzila kuwa na vitanda vya kulaza wagonjwa visivyopungua 300, huku likigharimu shilingi za kitanzania bilioni 30”, alisema Dkt. Naizhijwa


Dkt. Naizhijwa alisema kwa sasa JKCI inafanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kutokana na idadi ya vitanda vilivyopo katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na vitanda vilivyopo wodini lakini jengo jipya la JKCI litakalojengwa eneo la mloganzila likikamilika idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji itaongezeka.


“Kwa sasa JKCI inahudumia wagonjwa wa nje takribani 500 kwa siku, upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kwa mwaka tunafanya kwa wagonjwa 400 tofauti na mwanzo tulivyoanza tulikuwa tukifanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 100 kwa mwaka”, 


Jengo la JKCI litakalojengwa eneo la mloganzila likiisha litatupa fursa ya kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa wengine 400 kwa mwaka hivyo kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo wanaohitaji huduma za ujasauaji wa moyo”, alisema Dkt. Naizhijwa

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari