Milioni 950 zaokolewa kwa watoto 37 kufanyiwa upasuaji nchini
Na: JKCI
************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha
shilingi milioni 950 ambazo Serikali ingetumia kama watoto 37 wenye magonjwa ya
moyo ya kuzaliwa nayo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi maalumu ya siku tano
ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa
afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirikal la Mending Kids
lililopo nchini Marekani Daktari bingwa wa upasujai wa moyo kwa watoto wa JKCI Godwin
Sharau alisema watoto 16 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kuziba matundu,
kurekebisha valvu za moyo na mishipa ya damu ambayo haikuwa sawa.
Dkt. Godwin alisema kama watoto hao 16 waliofanyiwa upasuaji
mkubwa wa moyo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu gharama za
kupatiwa matibabu yao zingekuwa shilingi milioni 250 wakati matibabu hayo kwa
kufanyika JKCI yamegharimu kiasi cha shilingi milioni 90 na baadhi ya watoto
kupatiwa msamaha wa matibabu kutokana na hali zao za kiuchumi kutomudu gharama
za matibabu.
“Katika kambi hii tumeweza kuwafanyia upasuaji mkubwa wa moyo
watoto wa umri tofauti kuanzia mwezi mmoja hadi miaka mitano ambapo mtoto wa
mwezi mmoja alikuwa na matatizo manne katika moyo wake ikiwemo tundu katika
vyumba vya juu vya moyo, tundu katika vyumba vya chini vya moyo, mishipa
inayorudisha damu kutoka kwenye mapafu kupeleka damu upande wa kulia wa moyo
badala ya kuipeleka upande wa kushoto na mshipa wa PDA unaotakiwa kujifunga
baada ya mtoto kuzaliwa kutokujifunga”, alisema Dkt. Godwin
Dkt. Godwin alisema huu ni mwaka wa kumi tangu Taasisi hiyo
ianze kushirikiana na Shirika la Mending Kids ushirikiano ambao umezaa matunda
mazuri kwani kila mwaka wataalam wa shirika hilo wanavyofika JKCI ufika na
mbinu mpya za matibabu pamoja na kutoa vifaa vya matibabu kwa watoto bila
gharama.
“Upasuaji wa moyo kwa watoto katika nchi zilizoendelea umepiga
hatua sana, Taasisi yetu inakuwa kwa kasi katika kutoa huduma za upasuaji wa
moyo kwa watoto ndio maana tunaendelea kufanya ushirikiano na nchi zilezoendelea
lengo likiwa kukuza ujuzi wetu pamoja na kuwa na ubora wa huduma tunazozitoa
kwa wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Godwin
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema upande wa
matibabu ya upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab watoto 21 waliokuwa
na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu na mishipa ya damu
iliyobana wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Dkt. Stella alisema matibabu ya upasuaji mdogo wa moyo kwa
watoto 21 yamegharimu chini ya shilingi milioni 100 kwa kufanyika hapa nchini
tofauti na watoto hao kama wangepelekwa nje ya nchi matibabu yao yangefika
kiasi cha shilingi milioni 700.
“Tunaishukuru Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma za afya
zikiwemo huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na
kupunguza idadi ya watoto wanaopelekwa nje ya nchi kwani kwa kufanya hivyo
imeweza kuokoa fedha nyingi ambazo zingehitajika kwa ajili ya matibabu nje ya
nchi”, alisesma Dkt. Stella
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa upasuaji wa tundu
dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa watoto kutoka Shirika la Mending Kids
lililopo nchini Marekani Darren Berman alisema madaktari kutoka shirika hilo
wataendelea kushirikiana na madaktari wa JKCI kwa karibu, kubadilishana ujuzi na
kuwasaidia watoto wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo.
“Kupitia kambi zetu za matibabu ya moyo hapa JKCI tumeweza
kuwasaidia watoto wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu na kwa wiki
hii tumeweza kumfanyia upasuaji wa tundu dogo mtoto wa miezi nane aliyekuwa na
tundu kwenye moyo ambapo kupitia matibabu tuliyompa tumeweza kuokoa maisha
yake”, alisema Dkt. Darren
Dkt. Darren Berman alisema utaalamu wa kutoa huduma za
upasuaji wa moyo kwa watoto JKCI umeongezeka hivyo sasa hakuna haja ya watoto
watanzania wenye magonjwa ya moyo kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Naye mama ambaye mtoto wake amepatiwa matibabu katika kambi
hiyo Prisca Elius aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kumsaidia
mtoto wake kupata matibabu kupitia kambi hiyo kwani hakuwa na uwezo wa
kugharamia matibabu ya mtoto wake.
Prisca alisema baada ya kuambiwa kuwa mtoto wake ana tatizo
la moyo alipoteza matumaini kwani hakujua ni kwa namna gani angefika Dar es
Salaam na angepata wapi fedha kwa ajili ya matibabu.
“Nawaomba madaktari wa JKCI na wenzenu kutoka nchini Marekani
muendelee kuwa na moyo huu wa kutusaidia sisi tusiokuwa na uwezo, mmetusaidia
sana maana nilishaambiwa tatizo alilokuwa nalo mwanangu nisipomtibu
nitampoteza, nawashukuru sana”, alisema Prisca
Comments
Post a Comment