JKCI yawapeleka wataalamu wake nchini India kujifunza upasuaji wa kubadilisha Valvu bila kufungua kifua

Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa
ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa nchini India kwaajili ya kujifunza upasuaji wa
kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) pasipo kufanya
upasuaji wa kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure –
TAVI). Upasuaji huo unafanyika kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab
ambao ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwaajili ya kufanya uchunguzi na
matibabu ya moyo.
**************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wako nchini India kwaajili ya kujifunza upasuaji wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) pasipo kufanya upasuaji wa kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI).
Upasuaji huo unafanyika kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo
wa Cathlab ambao ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwaajili ya kufanya
uchunguzi na matibabu ya moyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu leo jijini
Dar es Salaam daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI ambaye yuko nchini
India katika mafunzo hayo Khuzeima Khanbhai alisema upasuaji wa aina hii
haufanyiki hapa nchini lakini kutokana na teknolojia ya matibabu kukuwa Taasisi
hiyo imeona iwapeleke wataalamu wake kujifunza nchini India.
“Tuko wataalamu wanne ambao kwa muda wa wiki moja tutakuwa
hapa India kujifunza aina hii ya upasuaji, wawili ni madaktari, muuguzi mmoja
na mtaalamu wa kuendesha mtambo wa Cathlab mmoja,.
“Upasuaji huu haufanyika hapa nchini kwani ni teknolojia mpya
na ya kisasa ya matibabu ya moyo ambayo inatumika katika nchi zilizoendelea
lakini kwakuwa katika Taasisi yetu tunavifaa vya kisasa Serikali imeona ni
muhimu na sisi tukajifunza ili tuweze kutoa huduma hii kwa watanzania wenye
matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Khuzeima.
Dkt. Khuzeima alisema upasuaji wa TAVI unafanyika kwa
wagonjwa wenye matatizo ya Valvu za moyo wenye umri wa kuanzia miaka 70 na
kuendelea au kwa watu ambao ni wagonjwa sana na hawawezi kustahimili upasuaji
mkubwa wa kufungua kifua.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inafanya upasuaji wa
kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) kwa njia ya upasuaji
mkubwa wa moyo wa kufungua kifua. Kuanza kufanyika kwa upasuaji mdogo wa TAVI
kutawasaidia wagonjwa wenye umri mkubwa au wagonjwa sana na hawawezi
kustahimili upasuaji mkubwa wa kufungua kifua kufanyiwa upasuaji huo hapa nchini na hivyo Serikali kupunguza
gharama za kuwapeleka wagonjwa hawa kutibiwa nje ya nchi.
Comments
Post a Comment