Wapewa mafunzo ya kutambua viashiria vya hatari katika utendaji kazi
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Martin Rubamba akichangia mada wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari katika utendaji wa kazi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira na sura mbalimbali kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa JKCI hivi karibuni.
Mteknolojia wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Mariam Steven akichangia mada wakati wa mafunzo ya siku mbili ya
kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari katika utendaji wa
kazi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira na sura mbalimbali kwa wafanyakazi
wa Taasisi hiyo hivi karibuni.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakisikiliza wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kutambua viashiria mbalimbali
vinavyoweza kusababisha hatari katika utendaji wa kazi vinavyoweza kujitokeza
katika mazingira na sura mbalimbali yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi
wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti na Ubora wa Huduma wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizhijwa Majani akiwa katika picha ya pamoja
na wafanyakazi wa Taasisi hiyo mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya siku
mbili ya namna ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari
katika utendaji wa kazi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira na sura
mbalimbali yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa JKCI.
Picha na: JKCI
******************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepewa
mafunzo ya siku mbili ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari
katika utendaji wa kazi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira na sura
mbalimbali.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa wafanyakazi wote wa
Taasisi hiyo yameanza kutolewa kwa wafanyakazi 50 ambao ni risk champions katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkuu wa Kitengo cha
Udhibiti wa Ubora wa Huduma wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Naizhijwa
Majani alisema mafunzo hayo ambayo ni yakwanza kufanyika yametolewa kwa kundi
la kwanza la wafanyakazi 50 ambapo baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo
wafanyakazi wote watapewa muongozo wa namna bora ya kudhibiti vihatarishi
katika Taasisi hiyo.
“Nia yetu kubwa ni
kuhakikisha wagonjwa wetu, wafanyakazi wa JKCI na wageni wote wanaofika katika
Taasisi yetu wanakuwa salama wakati wote”, alisema Dkt. Naizhijwa
Dkt. Naizhijwa alisema JKCI ina maono ya kuwa Taasisi ya
kimataifa katika kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo
nchini pamoja nchi zilizopo barani Afrika hivyo ni muhimu kukabiliana na
vihatarishi vinavyoweza kukwamisha Taasisi kufikia malengo yake.
“Ili tuweze kuwa katika viwango vya juu vya kutoa huduma za
matibabu ya moyo kimataifa lazima tuwe imara na kuweka mifumo ambayo
itatusaidia kujiandaa kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza”,
alisema Dkt. Naizhijwa
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM) Dkt. Indiael Kaaya alisema msingi wa mafunzo ya
udhibiti wa vihatarishi hujengwa ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia
malengo ya Taasisi.
Dkt. Kaaya ambaye pia ni mshauri na mtafiti alisema mafunzo
hayo yatawasaidia washiriki kujipanga na kuona uwepo wa kesho leo ili waweze
kutafakari yale ambayo wamekuwa wakifanya katika Taasisi hiyo na kuweka
mikakati ya kudhibiti vihatarishi kabla ya kutokea.
“Katika mafunzo haya tumepitia miongozo mbalimbali
inayotutaka kusimamia vihatarishi katika Taasisi za umma pamoja na kuangalia
mifumo rasmi inayosimamia udhibiti wa vihatarishi”, alisema Dkt. Kaaya
Dkt. Kaaya alisema mfumo wa usimamizi wa kudhibiti
vihatarisha unatoa muongozo wa namna ya kung’amua vihatarishi na kuunganisha
mpango wa udhibiti vihatarishi na mpango wa Taasisi kwa ujumla.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mtaalamu wa Tiba
Mionzi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Amani Materu alisema kupitia
mafunzo hayo ameweza kujifunza vitu vingi ikiwemo kutambua na kudhibiti
vihatarishi endapo vitatokea katika eneo lake la kazi.
Materu alisema upande wake kama mtaalamu wa tiba mionzi
ameweza kuainisha vihatarishi vinavyoweza kumrudisha nyuma katika utendaji wake
wa kazi kama hatazua vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika kazi zake za
kila siku.
“Kitu kikubwa kinachoweza kukwamisha malengo katika eneo
langu la kazi ni kuharibika kwa mashine, kutokea kwa hitilafu za umeme na
mifumo ya utumaji wa majibu ya mgonjwa, kwa kutambua vyanzo hivyo tutaenda
kuchukua hatua za mapema ili kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza
kujitokeza”, alisema Materu
Materu alisema mafunzo hayo yanaenda kuwa rafiki katika eneo
lake la kazi lakini pia kumsaidia hata nje ya eneo la kazi ikiwemo katika
familia yake pamoja na jamii iliyomzunguka.
Mafunzo hayo kwa awamu ya pili yanatarajiwa kufanyika
mwishoni mwa mwezi Oktoba ambapo wafanyakazi 200 wa JKCI watashiriki na awamu
ya tatu yatafanyika mwakani Januari ambapo wafanyakazi wengine 200 watashiriki.
Comments
Post a Comment