Wapigwa msasa wa kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo


Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Chuo Kikuu cha Brescia kilichopo nchini Italia kumfanyia upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab mgonjwa ambaye ana matatizo ya hitilafu katika msukumo wa damu wakati wa kambi maalumu ya siku tatu iliyoanza leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na: JKCI

*********************************************************************************************************

Wataalamu wa magonjwa ya moyo na  mfumo wa umeme wa moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanapewa mafunzo kwa vitendo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanatolewa na Prof. Antonio Curnis ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka chuo kikuu cha Brescia kilichopo nchni Italia.

Prof. Curnis alisema lengo la mafunzo hayo ni kubadilishana ujuzi wa kazi wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi, wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo pamoja na kufundisha teknolojia mpya ya jinsi ya kutoa matibabu hayo.

“Wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi kama watatibiwa mapema na vizuri wanaweza kuishi muda mrefu zaidi ya miaka 10 na hivyo kuokoa gharama za matibabu yao,  lakini kama watachelewa kupata matibabu na hawatapata matibabu mazuri muda wao wa kuishi huwa ni mfupi”,.

“Mimi na wenzangu tumekuja Tanzania kutoa mafunzo haya kwa wataalamu wa hapa nchini ili wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi na wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo waweze kupata matibabu mapema na kwa wakati”,  alisema Prof. Curnis.

Alizitaja sababu za moyo kushindwa kufanya kazi kuwa ni pamoja na mishipa ya damu ya moyo kuziba, msongo wa mawazo, shinikizo la juu la damu, kisukari, unywaji wa pombe kupita kiasi na matatizo ya ujauzito na dalili zake ni mgonjwa kushindwa kupumua na mapigo ya moyo kupungua tofauti na inavyotakiwa kuwa.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye alisema mafunzo hayo yatawasaidia kupata ujuzi wa jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi.

“Mafunzo haya yatatuwawezesha wataalamu wa JKCI na wenzetu wa nchini Italia kushirikiana kwa pamoja na kubadilishana uzoefu wa kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu ya mapigo ya moyo na moyo kushindwa kufanya kazi”, alisema Dkt. Gandye.

Dkt. Gandye alisema licha ya mafunzo hayo kufanyika kwa njia ya vitendo pia yanatoa nafasi kwa  wagonjwa sita kupata huduma ya matibabu  itakayowasaidia kupandisha  mapigo ya moyo na kuwezesha mioyo yao kufanya kazi vizuri kwa kupandikizwa vifaa visaidizi vya moyo ambavyo ni Pacemaker na Cardiac Resynchronization Therapy Device - CRTD.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano wa JKCI, Kas Medics Limited, Abbott na Chama cha madaktari katika tiba ya hitilafu ya mapigo ya moyo (Device and Arrhythmic Society of Tanzania – DAR Tanzania)  ambao walichagua wataalamu kutoka hospitali inayotibu wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo ili waweze kutoa mafunzo hayo kwa wataalamu wa hapa nchini.

Katika mafunzo hayo Abbott na Kas Medics Limited wametoa msaada wa vifaa tiba ambavyo ni Pacemaker na Curiously Recurring Template Pattern (CRTP) vyenye  thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60.

Mafunzo hayo yanakwenda sambamba na kongamano la siku moja litakalofanyika kesho tarehe 31 Oktoba jijini Dar es Salaam litakalokuwa na mada za moyo kushindwa kufanya kazi na mapigo ya chini ya moyo ambalo limewalenga  madaktari wote Tanzania hususani wanaohusika na utoaji wa tiba ya moyo ili waweze kutoa huduma za matibabu hayo pindi watakapokutana na wagonjwa wa aina hiyo.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari