JKCI wafanya utalii wa ndani msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika lango la kuingia kwenye msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani walipotembelea msitu huo hivi karibuni kwaajili ya kufanya utalii wa ndani na kujionea vivutio vilivyopo katika msitu huo.
Muongoza Watalii kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Peter Masome akiwaeleza Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) aina ya miti ya asili iliyopo ndani ya msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani wakati wafanyakazi hao walipofanya utalii wa ndani hivi karibuni katika msitu huo.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wamefanya utalii wa ndani wa kutembelea msitu
wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumzia kuhusu utalii huo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema wafanyakazi
wa Taasisi hiyo siku ya Jumamosi
waliamua kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za
kuhamasisha utalii na kwenda kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.
Dkt. Kisenge alisema wafanyakazi wa JKCI wanafanya kazi
katika mazingira ya huruma ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo mbalimbali
kwa kufanya kwao utalii katika msitu huo kumewafanya wajifunze vitu vingine
vipya tofauti na vile wanavyokutana navyo kazini pamoja na kujiburudisha.
“Tumewaleta wafanyakazi wetu kutalii katika msitu huu na
kuona mazingira tofauti na yale waliyopo
kila siku ya kuwahudumia wagonjwa kwa
kufanya hivi kutawapa ari mpya ya
kufanya kazi pamoja na kutangaza utalii uliopo kwa wagonjwa tunaowahudumia
kwani Taasisi yetu ina wahudumia wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi “, alisema
Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake muongoza watalii kutoka Wakala wa Misitu
Tanzania (TFS) Magdalena Lukumay alisema siku ya Jumamosi waliwapokea watalii
wa ndani kutoka JKCI ambao walitembelea
msitu huo na kuona vivutio mbalimbali vilivyopo.
Magdalena alisema ni mara chache wanapokea kundi kubwa lenye
watalii wengi wa ndani kama ilivyotokea kwa JKCI na kuziomba Taasisi nyingine
za Serikali na zisizo za Serikali kuiga mfano huo na kuwapeleka wafanyakazi wao
kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.
“Katika msitu huu wa mazingira asilia wenyeji waliopo ni kabila
la Wazaramo, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa hii ikiwa ni pamoja na
ngoma za asili, matambiko yanayofanyika katika mapango ya mzimu wa Mavoga na
vyakula vya asili”, alisema Magdalena.
Nao wafanyakazi wa JKCI ambao walitembelea msitu wa mazingira
asilia Pugu Kazimzumbwi walishukuru kwa nafasi waliyoipata na kusema kuwa
imewasaidia kujifunza vitu vipya ambavyo hawakuwa wanavifahamu.
Theresia
Marombe ambaye ni Afisa Muuguzi wa JKCI alisema amefurahi kutembelea msitu huo na ni mara
yake ya kwanza kufika mahali hapo amefurahi zaidi kuona wafanyakazi wote
wamekaa pamoja katika mazingira ya asili na kujifunza mambo mbalimbali.
“Kuna
umuhimu wa watanzania kutenga muda wa kutembelea vivutio vya utalii tulivyonavyo na kuona vitu
vya asili , kuja hapa ni mara yangu ya kwanza nitawaambia na wenzangu waje hapa kuona
miti, popo na ndege wa asili waliopo
hapa”, alisema Theresia.
“Ninashukuru kupata nafasi ya kutembelea msitu wa
mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi nimeona vitu ambavyo mjini havipo lakini hapa
vipo, ninatoa wito kwa watanzania wenzangu wafanye utalii wa ndani kama huu
tulioufanya siku ya leo na kuona vitu vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia
Watanzania kuwa navyo”, alisema Herry
Magwaza ambaye ni Mtunza Kumbukumbu wa JKCI.
Wakiwa katika msitu huo wafanyakazi hao walipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na bwawa la Minaki lenye kina cha mita nane na urefu wa kilomita 1.2, mapango ya popo, pango la mzimu wa Mavoga, kupanda mlima wenye urefu wa kilomita 1.5 kwa kutumia kamba pamoja na kuona miti ya asili , ndege, vipepeo na panzi wenye bendera ya taifa.
Comments
Post a Comment