Wafanyakazi JKCI wametakiwa kuwa wabunifu na kutumia utaalamu walionao kuwahudumia wagonjwa
Afisa Uuguzi mstaafu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Fatihiya Mustafa akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge zawadi ya picha ya saa ya ukutani kwaajili ya wafanyakazi wanaofanya kazi katika chumba cha kutoa huduma ya vipimo vya moyo vya ECHO na ECG wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika hivi karibuni katika msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wametakiwa kuwa wabunifu na kutumia utaalamu walionao kwa kuwahudumia wagonjwa
kwa kufanya hivyo watakuwa wameisadia Serikali ambayo imetumia fedha nyingi
kuwasomesha na kununua vifaa tiba vya kisasa vya kutibu magonjwa ya moyo.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi
wa Taasisi hiyo ya jinsi ya kufanya kazi kimkakati na kufikia malengo
waliyojiwekea yaliyofanyika katika msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi
uliopo Kisarawe mkoani Pwani.
Dkt. Kisenge alisema ubunifu
mahali pa kazi unasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza na hivyo kufikia
dira ya Taasisi hiyo ya kuwa Taasisi inayotambulika kimataifa katika kutoa
huduma, mafunzo na utafiti wa moyo.
“Ninawaomba mfanye kazi kwa bidii huku mkifuata maadili ya
kazi yenu ya kuwahudumia wagonjwa kwani kazi hii inahusisha maadili , fanyeni
kazi kwa pamoja na kutumia utaalamu mlio nao
kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”.
“Tumeamua kufanya mafunzo haya katika msitu huu mahali ambapo
ni nje kabisa ya eneo la kazi ili wafanyakazi waweze kuelewa kirahisi vitu
vinavyofundishwa ambavyo vitawasaidia katika utendaji wao wa kazi za kila
siku”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya
Uongozi Dunstan Mulaku alisema amewafundisha
wafanyakazi hao namna ya kufanya kazi kimkakati na kufikia malengo
waliyojiwekea kwa kufanya hivyo wataisaidia JKCI kufika mbali zaidi.
Mulaku alisema maadili ya msingi ya Taasisi hiyo ni
ushirikiano, uadilifu, weledi na ubunifu kama wafanyakazi hao watayafuata
wataweza kufikia malengo ya Taasisi ya kutoa huduma za moyo zenye uthibitisho, mafunzo na utafiti.
Kwa upande wa wafanyakazi walioshiriki mafunzo hayo
walishukuru kwa nafasi waliyoipata ya
kushiriki mafunzo na kusema kuwa imewasidia kujua mbinu za kufanya kazi
kimkakati na kufikia malengo waliyojiwekea.
Dkt.Tulizo Shemu ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI
Dar Group alisema mafunzo hayo yameenda sambamba na maadhimisho ya miaka nane
ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo na wafanyakazi
wamefundishwa jinsi ya kufanya kazi kama timu ili wafikie malengo ya
miaka mitano kama yalivyopangwa katika mpango mikakati.
Monica Mwaluka ambaye ni daktari kutoka Hospitali ya JKCI Dar
Group alisema amefurahi kuungana na wafanyakazi wa JKCI makao makuu kwa pamoja wamepata mafunzo na
kufanya utalii wa ndani katika msitu huo wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi kwa
kuwa kwao karibu wataweza kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.
“Ninaushukuru uongozi kwa kuandaa mafunzo haya ambayo
yameniwezesha kujua mbinu za kufanya kazi kimkakati huku nikishirikiana na
wenzangu hakika yatanisaidia katika
utendaji wangu wa kazi za kila siku”, alisema Dkt. Monica.
“Mafunzo haya yamenifanya niweze kujitambua na kujua jinsi ya
kufanya kazi na watu wenye tabia mbalimbali nitayatumia katika kutoa huduma kwa
wagonjwa ili wananchi wengi waweze kufaidika na Taasisi yetu iweze kusonga
mbele zaidi”, alisema Dominick.
Licha ya kushiriki mafunzo hayo wafanyakazi hao walipata nafasi
ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea
maeneo mbalimbali ya msitu huo ikiwa ni pamoja na bwawa la Minaki lenye kina
cha mita nane na urefu wa kilomita 1.2,
mapango ya popo, pango la mzimu wa Mavoga, kupanda mlima wenye urefu wa
kilomita 1.5 kwa kutumia kamba pamoja na kuona miti ya asili , ndege, vipepeo
na panzi wenye bendera ya taifa .
Comments
Post a Comment