Kwa mara ya kwanza JKCI Dar Group wafanya upasuaji mdogo wa moyo
Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group imefanya upasuaji mdogo wa moyo kuondoa maji yaliyokuwa
yameuzunguka moyo kwa wagonjwa ambao walikuwa na tatizo la maji kujaa kwenye mfuko
unaotunza moyo (pericardia effusion).
Upasuaji huo umefanyika kwa wagonjwa wawili ambao wameonekana
kuwa na dalili za magonjwa mengine yaliyopelekea mfuko unaotunza moyo kujaa
maji kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza kuhusu matibabu hayo Daktari Bingwa wa magonjwa
ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tawi la JKCI Hospitali ya Dar Group
Samweli Rweyemamu alisema wagonjwa hao maji yamekuwa yakijaa pole pole kwenye
mfuko unaotunza moyo ambapo mgonjwa mmoja maji yaliyotolewa yalifika kiasi cha
lita moja na nusu na mwingine mills 750.
Dkt. Rweyemamu ambaye pia ni Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Tiba
JKCI Hospitali ya Dar Group alisema kwa kawaida maji yaliyopo kwenye mfuko
unaotunza moyo huwa mills 50 hadi 100 lakini ikitokea yakaongezeka ghafla hadi kufukia
mills 200 na kuendelea mtu huanza kupata hali za tofauti katika mwili wake
ikiwemo kuchoka, mapigo ya moyo kwenda mbio na moyo kushindwa kufanya kazi
vizuri.
“Tiba ya tatizo la kujaa maji kwenye mfuko unaotunza moyo ni
kuyaondoa maji hayo ambapo kwa wagonjwa hawa tumeweza kuwatoa maji yaliyokuwa
yamezunguka mioyo yao na kuusababishia moyo kutaka kusimama”,
“Kiashiria kikubwa anachokuwa nacho mgonjwa ambaye maji
yamejaa kwenye mfuko unaotunza moyo anaweza kuwa na magonjwa mengine ambayo
yanaashiria ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hivyo kupelekea mfuko unaolinda moyo
kujaa maji”, alisema Dkt. Rweyemamu.
Dkt. Rweyemamu alisema maji yaliyotolewa kwa wagonjwa hao
yamepelekwa katika Maabara za juu kwaajili ya kuchunguza tatizo lililosababisha
maji kujaa lakini pia kuangalia kama kuna tatizo zaidi kutokana na maji hayo
kuwa na mchanganyiko wa damu.
“Mgonjwa mmoja tuliyemtolea maji alikuwa anapata changamoto ya
kupumua kutokana na maji kujaa eneo linalouzunguka moyo wake, pia oksijeni
kwenye mwili wake ilikuwa inashuka, na mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana”,
alisema Dkt. Rweyemamu.
Dkt. Rweyemamu alisema kutokana na tatizo walilokuwa nalo
wagonjwa hao la kujaa maji na mioyo yao kushindwa kufanya kazi vizuri kama wasingepatiwa
matibabu mapema wangeweza kupoteza maisha ghafla.
Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kuondoa maji
katika mfuko unaotunza moyo Hussein Mamboleo alisema kwa muda wa wiki mbili
zilizopita amekuwa akikosa nguvu na kusikia mapigo ya moyo kwenda kwa haraka
hivyo kufika JKCI Hospitali ya Dar group kwa ajili ya kuchunguza.
Hussein alisema baada ya uchunguzi na kugundulika kuwa moyo
wake umezungukwa na maji alipatiwa matibabu ya kuondoa maji hayo ambapo baada
ya matibabu amekuwa akifanya mazoezi ya kutembea na kutokujisikia tena kuchoka
kama ilivyokuwa hapo awali.
“Kwasasa nipo vizuri naweza kutembea umbali mrefu bila ya
kuchoka, nawapongeza Taasisi ya Moyo kuweza kusogeza huduma za matibabu ya moyo
karibu na wananchi kwani sisi watu wa Temeke sasa hatuna haja ya kwenda JKCI
upanga kwaaliji ya matibabu ya moyo”, alisema Hussein
Hussein alisema kupatiwa matibabu JKCI Hospitali ya Dar Group
kumeirahisishia familia yake kupata urahisi wa kumhudumia mgonjwa umbali mfupi
kutoka nyumbani.
JKCI Hospitali ya Dar Group imekuwa ikipokea wagonjwa wa moyo
kutoka maeneo mbalimbali ya Temeke na maeneo ya jirani hivyo sasa kuanza kutoa
huduma za upasuaji mdogo wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu hayo
kurahisisha upatikanaji wa huduma na kusogeza huduma karibu.
Comments
Post a Comment