Dkt. Mpango: Tanzania yapiga hatua matibabu ya moyo
Wagonjwa wa moyo zaidi ya 800 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa
moyo, na zaidi ya 2,000 kufanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa
cathlab kwa kipindi cha miaka miwili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Aidha Wagonjwa wa moyo zaidi ya laki mbili wamepatiwa
matibabu katika taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo kati yao
wagonjwa 2400 walitoka nchi za jirani za Comoro, Congo DRC, Kenya, Malawi,
Mozambique, Rwanda, Uganda na Zambia.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa kimataifa wa
magonjwa ya moyo leo mjini Zanzibar Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema kutokana na huduma zinazotolewa na
Taasisi hiyo, zimeweza kuifanya JKCI kuwa taasisi ya umma inayoongoza katika
kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati hivyo kuwavutia
wanataaluma kutoka nchi za jirani zikiwemo nchi za Malawi, Zambia na Rwanda
kujenga mashirikiano.
Mhe. Dkt. Mpango alisema kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Serikali imeweza kuokoa fedha nyingi takribani bilioni 63 fedha za
kitanzania zilizokuwa zinatumika kwaajili ya matibabu ya moyo nje ya nchi.
Mhe. Dkt. Mpango alisema kati ya mafanikio yaliyofanywa na
Taasisi hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo
ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan services ambayo imekuwa
ikitoa huduma ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo katika hospitali za
mikoa na kuwafikishia karibu huduma za matibabu ya moyo wananchi wanaohitaji matibabu
hayo.
Aidha Dkt. Mpango alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kupanua huduma za matibabu na kumtaka Waziri
wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kufuatilia gharama za ujenzi utakaofanyika Hospitali
ya JKCI Dar Group na kuziwasilisha serikalini mapema ili serikali iweze
kuwekeza katika ujenzi huo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema
serikali itaendelea kuwekeza kuboresha matibabu ya moyo nchini upande wa
majengo, kuwa na vifaa tiba vya kisasa vinavyofanana na vilivyopo nchi
zilizoendelea pamoja na kuwaendeleza wataalamu wa moyo kuwa mabingwa wabobezi.
“Serikali imetupa fedha shilingi za kitanzania bilioni 9
kwaajili ya kuajiri na kusomesha madaktari kuwa mabingwa wabobezi katika
masuala ya moyo na hii itahusisha wataalamu wa afya ambao ni madaktari wa
upasuaji, wauguzi, wafamasia, na madaktari wa usingizi”, alisema Mhe. Ummy
Mhe. Ummy alisema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za
Afrika inakabiliwia na changamoto kubwa ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo
magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu na saratani.
“Wakati serikali inawekeza kwenye matibabu tunao wajibu wa
kuwekeza kwenye huduma za kinga kwani kinga ni bora kuliko tiba, hivyo tusifanye
mzaha kwenye mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu kubadili mtindo
wa maisha na kushiriki katika mazoezi ya mara kwa mara kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza”,
“Hata tukijenga Jakaya Kikwete 200 kama watanzania
hatutabadili mtindo wa maisha hazitatosha hivyo tunapaswa kuwekeza kwenye
huduma za kinga kuwaokoa wale ambao hawajapata magonjwa ya moyo wasipate”, alisema
Mhe. Ummy
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeanzisha mkutano huo wa kisayansi kwa
wataalamu wa afya nchini ukiwa na lengo la kuwapa ujuzi wataalamu wa afya
nchini kuhusu magonjwa ya moyo.
“Mkutano wetu unahusisha huduma za awali kabisa ambazo
mgonjwa wa moyo anatakiwa kupata lengo likiwa kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo
kwani wengi wao hufika JKCI kwa kuchelewa”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema kupitia mkutano huo ulioanza na
kongamano la siku moja kwa vitendo kwa wataalamu wa afya wameweza kupatiwa
ujuzi wa kuokoa maisha, kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi (Echocardiography-ECHO) pamoja na mafunzo ya jinsi ya kuunganisha mishipa
ya damu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema ili kuendelea kusogeza huduma za
matibabu karibu na wananchi JKCI inaenda kusimamia kitengo cha moyo
kilichowekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, kuhimarisha huduma za
matibabu ya moyo Hospitali ya Benjamini Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Bugano, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Rufaa ya
Kanda Mbeya.
Comments
Post a Comment