Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo kufanyika Zanzibar
Wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali nchini wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kumhudumia mgonjwa wa dharura wakati wa kongamano leo kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar
Na: JKCI
*****************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya mkutano wa
kimataifa wa magonjwa ya moyo kwa wataalamu wa afya nchini kuwapa mbinu
mbalimbali za kutambua wagonjwa wa moyo.
Mkutano huo ulioanza leo na kongamano la kutoa huduma
mbalimbali za magonjwa ya moyo kwa wataalamu wa afya utafanyika tarehe 9 na 10
katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Hotel ya Verde
iliyopo Zanzibar Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge alisema lengo la mkutano huo ni kuwawezesha madaktari wazawa
wa hospitali zote kuanzia ngazi za chini hadi taifa kubadilishana mawazo na
uzoefu kutoka kwa wataalamu wa JKCI na wenzao wa nje ya nchi.
Dkt. Kisenge alisema mkutano huo utawawezesha watu wa nchi za
Afrika kuielewa Taasisi hiyo na huduma zinazotolewa jambo ambalo litapelekea
kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
“Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia mkutano huu
unaenda sambamba na mafunzo maalumu kwa vitendo kwa madaktari wa upasuaji juu
ya mambo mbalimbali yakiwemo ya uvunaji wa mishipa ya moyo, jinsi ya kumhudumia
mgonjwa mahututi wakati wa kongamano kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo”,
alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema wawakilishi zaidi ya 500 ambao ni wazawa
na 40 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo ikiwemo
madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo na wauguzi wanaotoa huduma kwa wagonjwa
hao.
Aidha Dkt. Kisenge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza vifaa na rasilimali watu katika
Taasisi hiyo jambo ambalo limepelekea kuwa kimbilio la wagonjwa wa moyo kutoka
nchi mbalimbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa moyo kwa watoto Dkt. Godwin Sharau alisema katika mafunzo hayo watahakikisha wanagusa kile eneo linalohusiana na magonjwa ya moyo kutimiza lengo la mkutano.
Dkt. Godwin alisema wataalamu wa afya walioshiriki watapata
nafasi ya kujifunza changamoto za matibabu ya moyo, maendeleo mapya juu ya
ugonjwa wa moyo, upasuaji kwa kutumia tundu dogo, kuzibua mishipa ya damu
iliyoziba pamoja na kurekebisha mishipa ya damu iliyokinzana.
“Kwa wagonjwa wanaofika katika Taasisi yetu hadi sasa tunao
uwezo wa kuwahudumia lakini wapo wale ambao wana magonjwa ya moyo na hawafiki
katika taasisi yetu kwaajili ya matibabu ndio maana tunatoa mafunzo haya kwa
wenzetu kuwasaidia wale ambao hawafiki katika Taasisi kupata matibabu”, alisema
Dkt. Godwin
Naye kaimu mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete Asha Izina alisema ili kuhakikisha teknolojia zinatumika kwa
usahihi ni lazima kuwe na watu wenye uwezo wa kuzitumia ili kuhakikisha huduma
bora zinazotolewa kwa walengwa.
“Mkutano wetu utazungumzia huduma za moyo katika nchi za
Afrika sambamba na mafunzo mbalimbali yatakayowasilishwa na madaktari bingwa
kutoka ndani na nje ya nchi kuwasaidia
wataalamu wa afya kutoa huduma bora na kuijengea uelewa jamii kujua viashiria
vya magonjwa ya moyo”, alisema Asha
Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wenye kauli mbiu “Maendeleo
ya matibabu ya moyo katika nchi za Afrika utafunguliwa rasmi kesho na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na kufungwa
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi siku ya Jumamosi tarehe 10 Februari 2024.
Comments
Post a Comment