NHC yatakiwa kukamilisha ujenzi wa jengo la JKCI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi Mhe. Dkt.
Faustine Ndugulile Mbunge wa Kigamboni akuzungumza
na vyombo vya habari wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili
ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************Kamati ya kudumu ya bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka mradi wa ujenzi wa jengo la utawala na vipimo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile Mbunge wa Kigamboni wakati wa
ziara ya kamati hiyo waliyoifanya JKCI kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za
matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mhe. Dkt.Ndugulile alisema katika ziara hiyo wametembelea
maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo, wamezungumza na wagonjwa ambao wanafurahia huduma wanazozipata
na kuona huduma zinazotolewa lakini wamekutana na changamoto ya ufinyu wa
miondombinu katika eneo la kusubiria wagonjwa, eneo la vipimo na vyumba vya kulala wagonjwa.
“Tanzania tunayotaka kwenda nayo siyo ya wagonjwa kulala
wengi katika chumba kimoja kwani dunia inakoelekea kila mgonjwa aliyelazwa
hospitali atalala katika chumba chake ninaamini
kukamilika kwa jengo hili la ghorofa nne kutasaidia kupunguza changamoto ya
nafasi katika Taasisi hii”.
“Kazi hii ya ujenzi imechukuwa muda mrefu kukamilika ilibidi ikamilike mwezi wa tano mwaka jana lakini hadi sasa ujenzi bado
haujakamilika na malipo yao yako tayari,
ninaiagiza wizara ya afya wafanye kazi kwa ukaribu ya kusimamia watu waliopewa
kazi hii ili wakamilishe mapema na huduma ianze kutolewa”, alisema Mhe.Dkt. Ndugulile.
Aidha kamati hiyo imeridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa
JKCI kwani imefanya mapinduzi makubwa ndani ya miaka 10 asilimia 90 ya
wagonjwa waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kutibiwa hivi sasa wanatibiwa hapa nchini na
aslimia 95 ya wagonjwa wa moyo
wanatibiwa hapa nchini.
Mhe. Dkt. Ngugulile alisema kupatikana kwa huduma bora za kibingwa za matibabu ya moyo hapa nchini
kumewafanya wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja kuibiwa na hivyo kuhamasisha
utalii wa matibabu.
Alimpongeza Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo
hapa nchini kwa kuboresha majengo, kusomesha
wataalamu na kununua vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu aliishukuru
kamati hiyo kwa kufanya ziara yao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
kujionea kwa macho huduma wanazozitoa, kuzungumza na wagonjwa pamoja na kufahamu changamoto zilizopo.
Mhe. Ummy alisema katika nchi za Afrika ukiondoa Afrika ya
Kusini na Misri Tanzania inafanya vizuri katika matibabu ya moyo. Hivi karibuni alikutana
na wadau wa afya kutoka nchini Marekani ambao
walisema watashirikiana na JKCI na kuhakikisha inakuwa kituo kikubwa cha
matibabu ya moyo barani Afrika ila waliomba
huduma hizo zisambae zaidi mikoani .
“Ili kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu
na wananchi ni muhimu JKCI ikaanzisha
matawi mikoani katika kanda zote lakini
kipaumbele kiwe kanda ya ziwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ili wataalamu
wajengewe uwezo na kutoa huduma za
kibingwa za matibabu ya moyo na wananchi wengi zaidi watafikiwa na huduma hizo”,
alisisitiza Mhe. Ummy.
Aidha Mhe. Ummy alisema wataalamu wa afya wamekuwa wakifanya
kazi nzuri ya kuokoa maisha ya wagonjwa ila inapotokea changamoto kidogo katika
utoaji wa huduma wamekuwa wakilaumiwa jambo ambalo linawavunja moyo, lakini wizara imekuwa ikiwachukulia hatua wale
wote wanaokwenda kinyume na kanuni na miongozo ya matibabu.
”Ninaomba tuwatie moyo wataalamu wa afya tusiwavunje moyo kwani
kazi wanayoifanya ni ngumu tukiwatia moyo wataona tuko pamoja na tunawajali,
kuna baadhi ya watumishi wa afya ambao wanafanya kazi zao kinyume na maadili hawa
wote Wizara imekuwa ikiwachukulia hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na
kuwafutia leseni”, alisema Mhe. Ummy.
Waziri huyo wa Afya alisema kuanzishwa kwa huduma ya afyamtandao (telehealth) katika Taasisi hiyo
kutasaidia kupuguza gharama za mgonjwa
kusafiri kutoka mkoani na nje ya nchi kufuata huduma ya matibabu Dar es Salaam
kwa kutumia huduma hiyo ataweza kufanya consultation
na kupata huduma za matibabu na dawa
akiwa mbali na Hospitali.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikihudumia wastani
wa wagonjwa 400 hadi 500 kwa siku huku wagonjwa wanaolazwa wastani wake ukiwa
ni 100 kwa wiki.
Taasisi hiyo inatibu wagonjwa kutoka nje ya nchi huku wengi wao wakiwa ni kutoka katika nchi za
Malawi, Kongo, Zambia, Rwanda, Burundi, Visiwa vya Comoro, Kenya, Msumbuji,
Burundi pamoja na kutoka nchi za nje ya Bara la Afrika ambao wanakuja hapa
nchini kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za utalii .
“Ili kusongeza huduma kwa wananchi tumekuwa tukitoa huduma ya
tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafuata wananchi mahali walipo na kuwapa
elimu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kufanya upimaji na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa
tumetembelea mikoa 12”.
‘Katika mikoa 12 tuliyokwenda kutoa huduma za tiba mkoba tumeona wagonjwa zaidi ya 10000 kati ya hao
wagonjwa 2800 hawakuwa wanajijua kuwa na tatizo la ugonjwa wa moyo na wagonjwa
1000 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibau ya kibingwa na tuliwapa rufaa
ya kuja kutibiwa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipata ushirikiano wa kutosha kutoka Wizara ya afya kwani imekuwa ikiisimamia na kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Comments
Post a Comment