JKCI yafanya kliniki ya matibabu ya moyo mkoani Geita
Baadhi ya wakazi wa Geita wakiwa katika foleni ya kusubiri kupata huduma katika kliniki maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) iliyopo mkoani Geita. Jumla ya wagonjwa 312 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu katika kliniki hiyo iliyomalizika leo.
Na: JKCI
************************************************************************************************************
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wameweka kliniki maalumu ya matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo kwa
wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo mkoani Geita.
Kliniki hiyo maalumu ya wiki moja imefanyika katika Hospitali
ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) na kumalizika leo kwa kufanywa na wataalamu wa
afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa CZRH ambapo wagonjwa 312 wamefanyiwa
vipimo vya moyo na kupatiwa matibabu.
Kliniki hiyo inatarajiwa kufanyika mara moja kila mwezi lengo
likiwa kuwajengea uwezo wataalamu wa CZRH pamoja na kuiwezesha Hospitali hiyo
kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wagonjwa wa moyo
waliopo kanda ya ziwa.
Akizungumzia kliniki hiyo Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo
na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Williams Ramadhan alisema
kati ya watu 312 waliopatiwa huduma watu 13 wamekutwa na matatizo ya kuziba kwa
mishipa ya moyo, watu 12 wamekutwa na matundu kwenye moyo, na watu 14 wamekutwa
na matatizo ya umeme wa moyo (arrhythmias).
“Watu 55 tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu,
watu saba wana magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya damu ya miguu, watu sita wana
vidonda sugu kwasababu ya mishipa ya miguu kutanuka na kuwa na shinikizo la juu
la damu, na watu wawili tumewakuta na tatizo la kutanuka kwa mshipa mkubwa wa
aorta”, alisema Dkt. Ramadhan
Dkt. Ramadhan alisema wagonjwa 51 wamepewa rufaa kufika JKCI
kwaajili ya matibabu zaidi ambapo 13 watahitaji upasuaji wa kuzibua na
kupandikiza mishipa ya damu, wagonjwa 14 watahitaji kufungwa vifaa maalumu
kurekebisha mfumo wa umeme wa moyo, wagonjwa 11 kufanyiwa upasuaji wa mishipa
ya miguu, wagonjwa 12 kufanyiwa upasuaji wa kuziba matundu ya moyo na mgonjwa
mmoja kupandikizwa mshipa mwingine wa bandia.
Kwa upande wake Mratibu wa huduma za afya Hospitali ya Rufaa
ya Kanda Chato (CZRH) Dkt. Osward Lyaba alisema Hospitali hiyo ilianzisha
kliniki ya magonjwa ya moyo miezi sita iliyopita ambayo ilizinduliwa na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
marehemu Prof. William Mahalu.
“Katika kuendeleza huduma za kliniki hii wataalamu wa afya
kutoka JKCI wameshirikiana nasi kwa kuweka kambi ya wiki moja katika Hospitali yetu
ikiwa ni sehemu ya kutujengea uwezo na kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo
wanaohitaji huduma za kibingwa”, alisema Dkt. Osward
Dkt Osward alisema kambi hiyo imehusisha wataalamu wa afya
mabingwa wa matibabu ya moyo, mabingwa wa upasuaji wa moyo na wataalamu wa
vipimo vya magonjwa ya moyo.
“Mwitikio umekuwa mkubwa kwani kwa siku tatu za mwanzo
tumeweza kuona takribani watu 230 waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa
matibabu ya moyo na wale waliohitaji huduma zaidi wamepewa rufaa kufika JKCI
kwaajili ya matibabu zaidi”, alisema Osward
Comments
Post a Comment