Watu 587 wapimwa moyo Arusha
Watu 587 wamepimwa moyo wakati wa kambi maalumu ya siku sita
iliyofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
mkoani Arusha.
Kambi hiyo maalumu iliyomalizika hivi karibuni imefanyika
katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kuanzia
tarehe 19 Februari ambapo wananchi wa Arusha na mikoa ya jirani walipata fursa
ya kupima magonjwa ya moyo.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Rweyemamu alisema jumla ya
wanawake 364 sawa na asilimia 60 na wanaume 223 sawa na asilimia 40 walipatiwa
huduma za vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Dkt. Rweyemamu alisema baada ya watu hao kufanyiwa vipimo na
matibabu, watu 58 sawa na asilimia 10 walipewa rufaa kufika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya matibabu zaidi na wengine kwaajili ya
kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Asilimia 90 ya watu wote waliopatiwa matibabu katika kambi
hii tumewakuta na matatizo ya shinikizo la juu la damu ambapo baadhi yao tayari
wapo katika matibabu na wengine tumewagundua kwa mara ya kwanza”, alisema Dkt.
Rweyemamu
Akizungumza mara baada ya kupatiwa huduma katika kambi hiyo
mkazi wa Arusha Furaha Saitori aliwashukuru wataalamu wa afya kutoka JKCI kwa
kuweka kambi hiyo kuwasaidia wananchi wa Arusha ambao bila kambi hiyo
wasingepata nafasi ya kupima afya zao.
Furaha aliziomba hospitali za kibingwa nchini kuwapeleka
wataalamu wake maeneo mbalimbali nchini kutoa huduma kwa wananchi kwani wapo
wananchi wengi wana matatizo ya kiafya lakini hawawezi kuzifikia hospitali
hizo.
“Kwakweli wananchi wa Arusha tumefurahi sana kupitia kambi
hii tumepima moyo na kujijua, tunaomba na wataalamu wa magonjwa mengine
watufikia ili tuweze kupima afya zetu kwani wapo watu wanapoteza maisha kwa
kutogundua ugonjwa mapema”, alisema Furaha
Comments
Post a Comment