Wagonjwa 10 wafanyiwa upasuaji wa moyo
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu mgonjwa ambaye mshipa wake ulikuwa umeziba ((Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG) wakati wa kambi maalumu ya siku nne iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo
************************************************************************************************************
Wagonjwa 10 wenye matatizo ya mishipa ya damu kuziba, valvu za moyo kuziba pamoja na mshipa mkubwa wa moyo kutanuka (Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG) wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo.
Kambi hiyo maalumu ya siku nne iliyomalizika hivi karibuni imefanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi wa Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani.
Wagonjwa sita waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab na wengine wanne wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.
Akizunguma na mwandishi wa habari hii Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angela Muhozya alisema kambi hiyo imefanyika kwa mafunzo zaidi upande wa kupandikiza mishipa ya damu bila ya kuusimamisha moyo.
“Wataalamu wa Taasisi wamepata muda wa kufanya upasuaji wa kupandikiza mshipa mkubwa wa moyo bila ya kuusimamisha moyo na kupata utaalamu wa hali ya juu ambao utawasaidia kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia”,
“Tumefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa wa moyo wagonjwa watatu waliokuwa na tatizo la mishipa ya damu kuziba ambao tumewapandikiza mishipa mitatu na mwingine minne na mgonjwa mmoja tumemfanyia upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG)”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake daktari kutoka Shirika la Madaktari Afrika Stephen Dorazio alisema imekuwa wiki yake ya mafanikio kushirikiana na wataalamu wa afya wa JKCI kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliohitaji huduma ya upasuaji wa moyo kuokoa maisha yao.
Dkt. Stephen alisema ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania safari ambayo imemuwezesha kubadilishana ujuzi na wataalamu wa JKCI kuonyeshana mbinu mbalimbali za kuwatibu wagonjwa wanaohitaji kuzibuliwa mishipa ya damu na kupandikizwa mishipa.
“Nimefurahi kufanya kazi na wataalamu wa JKCI, mgonjwa tuliyempandikiza mshipa mkubwa wa damu upasuaji wake ulikuwa mgumu kidogo na kutuchukua masaa 12, tunashukuru sasa anaendelea vizuri”, alisema Dkt. Stephen
Akizungumzia kuhusu upasuaji mdogo wa moyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Salehe Mwinchete alisema wagonjwa sita wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kuzibua mishipa na valvu za moyo zilizoziba.
“Katika kambi hii tumemfanyia upasuaji wa kuzibua valvu ya moyo iliyoziba mama mwenye ujauzito wa miezi 8 pamoja na mtoto mwenye umri wa miaka 14 ambaye pia valvu yake ya moyo ilikuwa imeziba”, alisema Dkt. Mwinchete
Dkt. Mwinchete alisema baada ya kufanya matibabu ya kuzibua mishipa ya damu na valvu za moyo zilizoziba mgonjwa anakuwa amepata nafasi ya kutokufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kwa kipindi cha muda mrefu.
“Mgonjwa ambaye amezibuliwa valvu za moyo zilizoziba kama hatapata maambukizi mapya anaweza asifanyiwe kabisa upasuaji wa moyo, lakini pia kupitia upasuaji huu mgonjwa alazimiki kutumia dawa za kulainisha damu wala kuchoma sindano kwaajili ya kuzuia maambukizi ya donda koo”, alisema Dkt. Mwinchete
Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa tundu dogo katika kambi hiyo Vida Mwenda alisema amekuwa akipata dalili za kuchoka, kushindwa kupumua vizuri tangu mwaka 2022 baada ya kujifungua mtoto wake wa pili.
“Sasa nimebeba mimba nyingine, hapa ndio dalili zimezidi nikaona niende katika Hospitali ya Mkoa Iringa na baada ya kunichunguza wamenipa rufaa kufika JKCI ambapo nimefanyiwa upasuaji mdogo na ninaendelea vizuri”, alisema Vida
Vida alisema kuwa kwake na bima ya afya kumemrahisishia kupata matibabu kirahisi na kwa wakati hivyo kuishauri jamii kuwa na bima ya afya itakayowahakikishia kupata matibabu kirahisi pale wanapopata changamoto za kiafya.
Comments
Post a Comment