JKCI kushirikiana na Misri kuboresha matibabu ya moyo nchini
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na kampuni
ya STERI CARE iliyopo nchini Misri kurahisisha upatikanaji wa vifaa tiba vya
matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.
Ushirikiano huo utagusa eneo la vifaa tiba vya moyo, mavazi
yanayotumiwa na wataalamu wa afya eneo la kazi pamoja na kushirikiana katika
kubadilishana ujuzi wa kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Akizungumza wakati wa kikao na wadau kutoka kampuni ya STERI
CARE Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge alisema JKCI inatamani kuagiza vifaa tiba kutoka nje ya nchi moja kwa
moja kupunguza gharama za vifaa hivyo itakayopelekea gharama za matibabu
kupungua pia.
“Kama JKCI itapata makampuni makubwa nje ya nchi na kuchukua
mahitaji yake huko gharama za vifaa vinavyohitajika kwaajili ya matibabu ya
moyo zitapungua lakini pia kupunguza athari za ukosefu wa vifaa hivyo kwa
wakati”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema Taasisi itafanya utafiti yakinifu na
kuainisha viwanda mbalimbali vinavyotengeneza vifaa tiba ili iweze kufanya
navyo kazi kwani uhitaji wa vifaa tiba umekuwa mkubwa.
Naye mwakilishi kutoka kampuni ya STERI CARE iliyopo nchini
Misri Mohmad Tohan alisema kampuni hiyo ipo tayari kufanya kazi na JKCI kwani
huduma nyingi zinazotolewa na kampuni hiyo zipo JKCI.
“Leo tumekuja na mavazi ya wataalamu wa afya tuliyonayo ili
muweze kuona kazi zetu lakini pia tunavyo vifaa vinavyotumika katika matibabu
ya magonjwa ya moyo ambavyo tunaamini mkichukua kwetu gharama zitapungua”,
alisema Mohmad
Comments
Post a Comment