Kongamano la kwanza la shambulio la moyo kufanyika nchini






Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani kuhusu Mkutano wa shambulio la moyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 17-18  mwezi huu katika hoteli ya Bahari Beach Jijini Dar es Salaam.


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khuzeima Khanbhai akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa kwa kliniki ya maumivu ya kifua yenye lengo la kuhakikisha wagonjwa wa shambulio la moyo wanapata matibabu kwa wakati.


Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiwaeleza waandishi wa habari umuhimu wa kufuata mtindo bora wa maisha ili mtu aweze kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo. 

     Mkurugenzi wa matibabu ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akizungumzia na Waandishi wa Habari  kuhusu wagonjwa wa shambulio la moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************

 KONGAMANO la Kwanza la Shambulio la moyo litafanyika kesho Februari 17  na kumalizika Februari 18 jijini Dar es Salaam  huku washiriki kutoka nchi mbalimbali wakitarajiwa kutoa mada zitakazowajengea uwezo watoa huduma za afya hapa nchini.

 Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Peter Kisenge alisema kongamono hilo litajumisha  madaktari kutoka Tanzania hususani wa moyo, madaktari, mafundi sanifu wa moyo na wauguzi  wa idara ya wagonjwa mahututi na wa dharura.

 Dk Kisenge alieleza kuwa watakuwa na madaktari kutoka  Afrika mashariki na kati wa  nchi za Uganda,Kenya,Zambia,Uganda ,Rwanda na zingine.

 Aidha alisema Wawezeshaji katika kongamano hilo watatoka nchi za Marekani,Misri,India, Argentina na pamoja na madaktari bingwa wazawa watatoa mada kuhusu shambulio la moyo.

 "Matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi watu milioni 17 wanapoteza maisha na matatizo ya kuziba mishipa ya moyo yanaongezeka sana  duniani na yanachangia vifo ambapo kati ya watu 100, 000  asilimia 1.6 wanapoteza maisha.

 Aliongeza "Hapa nchi katika wagonjwa waliochunguzwa mishipa ya damu ya moyo  asilimia 6  walipata shambulio la moyo kama mgonjwa hatakuja haraka dakika 90 anaweza kupoteza maisha”.

 Dk. kisenge alibainisha kuwa wataendelea kufanya  mikutano hiyo ili madaktari wajue tatizo hilo na  watibu vizuri wagonjwa.

 Alisema Serikali imewekeza JKCI ambapo kuna mitambo miwili mikubwa ambayo gharama zake ni  Sh. bilioni 11 inayoweza kusaidia kutibu  matatizo hayo hivyo uwekezji ni mkubwa lakini bado madaktari hawana uelewa wa kutosha kuwasaidia wagonjwa wa shambulio la moyo.

 "Mkutano huu utafungua mkutano ambao utafanyika februari mwaka ujao ambapo wawakishi wa  nchi 40 watashiriki,tutaeleza dunia uwekezji mkubwa uliofanywa katika taasisi bora Afrika ya Mashariki na Kati,"alisisitiza Dk. Kisenge.

 Mkurugenzi wa tiba ya moyo JKCI Dk Tatizo Wanne alisema nia ya kongamano hilo  ni kuwajengea uwezo wataalamu mbalimbali kwani kutakuwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali na mikoa mbalimbali ya Tanzania. 

 Alisema Huduma za kutibu shambulio la moyo ziko sehemu mbili ikiwemo kutumia mitambo lakin sehemu nyingi hazina mitambo hivyo watawafundisha namna ya kuwasidia na kuwapeleka JKCI. 

 Mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo,Dk. Pedro Pallangyo alieleza kuwa tatizo la Shambulio la moyo linaongoza kusababisha vifo ambapo inakadiriwa watu milioni 200 wanakutwa na shambulio la moyo kila mwaka.

 Dk. Pallangyo Alisema watu hao asilimia kubwa wanapoteza maisha ambapo takwimu za karibuni watu wengi wanaopoteza maisha wanatokea kusini mwa jangwa la Sahara ambapo Tanzania ipo. 

 "Kama yalivyo magonjwa mengine yasiyoambukiza yanasababishwa na uvutaji wa sigara,uzito kupindukia,unywaji pombe kupindukia,kutofanya mazoezi la ulaji usiofaa hata shambulio la moyo linasababishwa na hayo.

 Alibainisha kuwa Moja ya sababu ya mkutano huo ni kupiga kelele kwa jamii kujua hili kwa kushirikiana na watoa huduma wengine.

 "Tumehamasisha jamii kufanya mazoezi kupitia kampeni za tembea na JKCI tunaamini jamii itapata uelewa mbali na kuwahi hospital kinga ni bora kuliko tiba wataepuka sababu hatarishi,"alifafanua. 

 Naye Daktari bingwa wa moyo ,Dk. Khuzeima Khanbhai alisema tangu mwaka jana wamezindua wodi ya wagonjwa wa maumivu ya kifua.

 "Anaweza kuja na kuhojiwa haraka kabla ya  dakika  90 anapelekwa kwenye mitambo na tunazibua mishipa baada ya saa 24 anaruhusiwa.

 

 

 



Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)