Wataalamu wa afya 300 washiriki kongamano la shambulio la moyo
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe akimsikiliza
Afisa Mauzo kutoka kampuni ya usambazaji wa dawa ya SUN PHARMA Innocent Maro
lipotembelea kuona huduma zinazotolewa na kampuni hiyo wakati wa kufunga
mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger
Plaza jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Khuzeima Khanbhai akipokea cheti cha kushiriki kuandaa mkutano
wa kwanza wa shambulio la moyo ulioandaliwa na Taasisi hiyo na kumalizika jana
jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya
Computech Limited Sandip Datta akipokea cheti cha kutambua mchango wake katika
kushirikiana na JKCI kufanikisha mkutano wa kwanza wa shambulio ya moyo kutoka
kwa Naibu Katibu Mkuu Dkt. Seif Shakalaghe wakati wa kufunga mkutano huo
uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari kutoka ITV Agnery Myala akipokea cheti
cha kukitambua chombo cha habari cha ITV kwa kushirikiana na JKCI kufanya kipindi cha kutangaza kuhusu ugonjwa wa shambulio la moyo wakati wa mkutano wa
kwanza wa shambulio la moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na kumalizika jana jijini Dar es Salaam. Vyombo vingine vya habari
vilivyopewa cheti kwa kushirikiana na JKCI kutangaza kuhusu shambulio la moyo ni pamoja na TBC, Channel 10, Star
TV, Clouds TV, Azam TV na ZBC
Picha na: Khamis Mussa na JKCI
**********************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetakiwa kuendelea
kufanya mikutano inayotoa mafunzo kwa wataalam wa afya itakayosaidia kuweka
mbinu za kujikinga na magonjwa yasiyo ambukiza pamoja na kutafuta namna ya
kutatua magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe wakati wa kufunga mkutano wa kwanza wa
Shambulio la moyo uliofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Larger Plaza
uliopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shakalaghe alisema mkutano huo umekuwa wa faida kwa
wataalam wa afya kwani sasa wataenda kuongeza jitihada za kuokoa maisha lakini
pia kuwapa nafasi wananchi kutambua dalili za ugonjwa huo hivyo kuchukua hatua
za haraka pale wanaposikia dalili za shambulio la moyo.
“Wizara ya Afya itahakikisha mikutano hii inafanyika kila
mwaka kuwakusanya wataalam wa afya maeneo tofauti ya dunia ili kwa pamoja
waweze kubadilishana ujuzi na kutatua tatizo la shambulio la moyo ambalo kwa
sasa linaonekana kuongezeka”,
Akizungumza katika Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Mkutano wa kwanza wa
shambulio la moyo umewahusisha wataalam wa afya 300 kutoka nchi mbalimbali
kujadili namna ya kuwahudumia wagonjwa wanaopata shambulio la moyo kwani sasa
limekuwa tatizo kubwa katika jamii.
“Tatizo la shambulio la moyo linasababisha vifo vingi, wagonjwa
wenye matatizo ya moyo duniani wanakaribia milioni 17 lakini wale wanaopata
mstuko wa ghafla wa moyo ni karibu milioni sita duniani kote na kati yao
asilimia 15 hupoteza maisha yao”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema shambulio la moyo hata hapa nchini lipo kutokana na mfumo wa maisha ya
kila siku ikiwemo uvutaji wa sigara, kutofanya mazoezi, kula mlo usio na afya,
kuwa na uzito uliopitiliza hivyo kupelekea matatizo ya moyo likiwemo shambulio
la moyo.
“Mkutano huu umewakutanisha wataalam wa afya ili kuona ni kwa
namna gani wataweza kuzuia tatizo la shambulio la moyo kwa kuwaelimisha
wananchi kufika mapema hospitali kwasababu mtu akipatwa na shambulio la moyo
anapaswa kufika hospitali mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu”,
“Tumeona tufanye mkutano huu uliowakutanisha wataalamu wa
afya kutoka nchi za Marekani, Agentina, Misri, India, Sudani, Kenya, Tanzania na
nchi nyinginezo kubadilishana ujuzi na kutengeneza mfumo wa kutambua matatizo
ya moyo na kuwaelimisha wataalamu wengine ambao hawakupata nafasi kushiriki
katika mkutano huu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema dalili za mstuko wa moyo ni pamoja na
kupata maumivu makali ya kifua yanayoenda hadi kwenye mkono na taya, kutokwa
jasho jingi, kukosa nguvu na kushindwa kupumua vizuri hivyo kuwataka wananchi
wanapopatwa na dalili hizo wafike kwa wataalam wa afya ili waweze kuchunguzwa
na kupatiwa huduma kwa wakati.
Naye mshiriki wa mkutano huo Daktari bingwa wa magonjwa ya
dharura na ajili kutoka hospitali ya KCMC Fransis Sakita aliipongeza JKCI kwa
kufikiria kuandaa mkutano huo ambao ungepaswa kufanyika siku za nyuma kwani
uhitaji wa taalama iliyotolewa katika mkutano huo ni hitaji kubwa kwa wataalam
wa afya.
Dkt. Fransis alisema kwa upande wa KCMC asilimia 22 ya
wagonjwa wa moyo waliowahi kuwaona walikuwa na tatizo la shambulio la moyo
hivyo kuona kuna uhitaji mkubwa wa jamii kuufahamu vizuri ugonjwa huo ili
waweze kujikinga.
“Katika Hospitali yetu mwanzo kulikuwa na uhaba wa vifaa vya
kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo lakini sasa hivi tumepata vifaa vya
kutosha pamoja na elimu ya mara kwa mara hivyo kutuwezesha kutambua wagonjwa na
kuwapatia huduma kwa wakati” alisema Fransis
Comments
Post a Comment