Wataalamu wa JKCI Waadhimisha siku ya wapendanao kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto 28



Wataalam wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya upasuaji wa kuziba tundu la moyo katika kambi maalum ya matibabu ya siku tano inayofanywa na wataalamu wazawa wa Taasisi hiyo ambapo watoto 28 walifanyiwa upasuaji.


Wataalam wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya upasuaji wa kuzibua mshipa wa damu wa moyo uliokuwa umeziba wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na madaktari hao ambapo watoto 28 walifanyiwa upasuaji.


Na: JKCI

*********************************************************************************************************

Watoto 28 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wazawa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

Kambi hiyo maalum ya upasuaji wa moyo ilifanyika kwa lengo la kusherehekea siku ya wapendanao itakayofanyika duniani kote tarehe 14 Februari mwaka huu ambapo wataalamu hao wameiadhimisha kwa kuonesha upendo wao kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo  kutokukaa katika mpangilio wake. 

Akizungumza wakati wa kambi hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo imefanyika mahususi kwa watoto wenye magonjwa ya moyo ili kuwapa upendo na kurejesha tabasamu kwao kwani watoto hao hupitia maumivu makali kutokana na maradhi waliyonayo. 

Dkt. Angela ambaye pia ni daktari wa usingizi alisema Idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo inaongezeka kila siku kwani watoto huendelea kuzaliwa, hivyo Idara ya upasuaji ikaona ni vizuri kufanya kambi hiyo huku lengo likiwa kupunguza idadi ya watoto hao wanaosubiria huduma ya upasuaji.

“Sisi kama madaktari pia ni wazazi na tumebarikiwa kuwa na watoto, tunaelewa mtoto anapokuwa mgonjwa wazazi wanakuwa kwenye wakati mgumu na  kupelekea baadhi ya mambo kwenye familia kusimama ndio maana tumeona ni vizuri kufanya kambi hii ili kupunguza idadi ya watoto wanaosubiri matibabu pamoja na kuwapa furaha”, alisema Dkt. Anjela . 

Naye Daktari wa bingwa wa upasuajiwa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa JKCI Godwin Sharau alisema katika kambi hiyo walifanya upasuaji wa  kuziba matundu kwenye moyo, kuachanisha mishipa iliyokaribiana pamoja na kuzibua mishipa iliyoziba. 

“Tumewafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto ambao mioyo yao ina matundu pamoja na wale ambao mishipa yao ya damu imeziba haipeleki damu vizuri kwenye moyo”,.

“Upasuaji tulioufanya katika kambi hii tumekuwa tukiufanya sisi kama wataalamu wazawa lakini kwa kufanya kambi maalumu tumewafikia watoto wengi zaidi kwa kipindi cha muda mfupi”, alisema Dkt. Sharau. 

Daktari huyo bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto alisema uzoefu wa madaktari wazawa wa upasuaji wa moyo kwa watoto umeongezeka kwani hapo awali kuna baadhi ya upasuaji kama wazawa walikuwa hawawezi kufanya lakini sasa wamebobea katika matibabu hayo bila hata ya kuwa na uangalizi kutoka kwa wenzao wa nchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya nao upasuaji huo.

Dkt. Sharau alisema kutokana na ufinyu wa wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo idadi ya watoto waliohudumiwa imekuwa chache lakini kama wodi hiyo ingekuwa kubwa watoto wengi zaidi wangefanyiwa upasuji huo.

“Watoto tuliowafanyia upasuaji wanaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi”, alisema Dkt. Sharau.

Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo waliishukuru JKCI kwa matibabu waliyayatoa kwa watoto wao na kuomba kambi kama hizo ziwe zinafanyika mara kwa mara ili watoto wengi zaidi waweze kutibiwa kwa muda mfupi. 

Rehema Yacob ambaye mtoto wake alizaliwa na tundu kwenye moyo pamoja na mshipa mmoja wa damu kutokupeleka damu vizuri kwenye moyo  alisema kama JKCI isingekuwepo hapa nchini asingeweza kumpeleka mtoto huyo nje ya nchi kutokana na kipato chake kuwa kidogo hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu. 

“Kutokana na ugonjwa huu wa moyo mtoto wangu alichelewa kutembea, lakini pia baada ya kutembea alikuwa akichoka mapema hivyo kushindwa kujumuika na wenzake kufanya michezo mbalimbali. Baada ya kufanyiwa upasuaji naona mabadiliko kwani sasa amechangamka na anafanya mazoezi”,.

“Kupitia changamoto za mwanangu niliona umuhimu wa kuwa na bima ya afya hivyo kutafuta bima hiyo ambayo imenisaidia kupata matibabu kiurahisi, nawashauri wazazi wenzangu kuwakatia watoto wao bima ya afya kwani matatizo huja ghafla”, alisema Rehema.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)