JKCI kutoa huduma za matibabu ya moyo nchini Malawi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe.Hamphrey Polepole wakati balozi huyo alipotembelea JKCI hivi karibuni kwa ajili ya kuona ni namna gani Taasisi hiyo itakavyotoa huduma ya matibabu ya moyo nchini Malawi.
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Hamphrey Polepole alipotembelea Taasisi hiyo hivi karibuni kwa ajili ya kuona ni namna gani Taasisi hiyo itakavyotoa huduma ya matibabu ya moyo nchini Malawi.
Picha na: Khamis Mussa
**********************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo
kwa wananchi wa Malawi mwishoni mwa mwezi wa tatu mwaka huu ili kuendeleza
mahusiano yaliyopo baina ya Tanzania na Malawi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokutana na Balozi
wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Hamphrey Polepole alipotembelea Taasisi hiyo kwa
ajili ya kuona ni namna gani Taasisi hiyo itakavyotoa huduma ya matibabu ya
moyo nchini humo.
Dkt. Kisenge alisema JKCI imekuwa ikiendelea vizuri tangu
ilipoanzishwa mwaka 2015 kwa kutoa huduma za tiba na upasuaji wa moyo kwa
wagonjwa hapa nchini pamoja na wagonjwa kutoka nchi za Comoro, Malawi,
Zimbambwe, Ethiopia, Kenya, Rwando, Burundi, Congo pamoja na nchi nyingine za nje
ya Afrika.
Dkt. Kisenge alisema Tanzania na Malawi imekuwa na mahusiano
mazuri kwani JKCI imekuwa ikiwapokea wagonjwa kutoka nchini humo kwa ajili ya
kuwahudumia hivyo basi umefika wakati kwa Taasisi hiyo kwenda kutoa huduma ya
matibabu nchini Malawi.
Aidha Dkt. Kisenge alimshukuru Mhe. Polepole kwa kutenga muda
wake na kutembelea Taasisi hiyo ili kwa pamoja waweze kushirikiana kupeleka
huduma za matibabu na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wa moyo waliopo nchini
Malawi.
“Nawahakikishia
wananchi wa Malawi kwa kufika hapa kwetu kupata huduma za matibabu watakuwa
wamechagua sehemu sahihi ambayo itawatatulia matatizo ya magonjwa ya moyo
yanayowakabili kwa gharama nafuu tofauti na wakienda sehemu nyingine duniani
kutafuta huduma hizi”, alisema Dkt. Kisenge
Naye Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Hamphrey Polepole
alisema uhusiano wa kimashirikiano ambao amekuwa akiupata kutoka JKCI umempa
motisha wa kuona umuhimu wa kufika katika Taasisi hiyo ili kwa pamoja waweze
kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha mahusiano ya afya upande wa matibabu ya
moyo kati ya Tanzania na Malawi.
“Kazi yetu ubalozini ni kufanyia kazi mahusiano ya Tanzania
na Malawi tukiangazia sera ya mambo ya nje, kwetu sisi tumeona Tanzania
imefanikiwa kujenga ubobezi kwenye sekta ya afya katika maeneo ya tiba ya moyo,
tiba ya mifupa na tiba ya figo hivyo kuanza kushirikiana na Taasisi hii
kusogeza huduma za matibabu ya moyo nchini Malawi”, alisema Mhe. Polepole
Mhe. Polepole alisema kwa sasa wananchi wa Malawi wanafuata
huduma za matibabu ya moyo nchini Afrika ya Kusini na India nchi ambazo zipo
mbali kidogo na nchi ya Malawi lakini pia gharama zake ni kubwa tofauti na
wagonjwa hao wangetibiwa Tanzania.
“Tumejipanga kwa kuanzia tutawakaribisha nchini Malawi mfanye
kambi ya matibabu ya moyo nchini humo ili wananchi wapate huduma ya matibabu
haya wakiwa nchini mwao na baada ya hapo waje kutibiwa nchini kwetu kama
ambavyo baadhi ya wananchi wa Malawi wanakuja kutibiwa hapana”, alisema Mhe.
Polepole.
Comments
Post a Comment