Wafanyakazi wapya JKCI wapewa mafunzo ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi
Mkufunzi wa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi na wadharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Afisa Muuguzi Samweli Mpiga akiwafundisha wauguzi wapya walioajiriwa katika Taasisi hiyo namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa mahututi leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa timu ya kuratibu jinsi ya kuokoa wagonjwa mahututi na
wadharura kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Faraji Lydenge
akiwaeleza wauguzi wapya walioajiriwa katika Taasisi hiyo umuhimu wa kutoa
huduma ya kwanza kwa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yamesimama wakati wa
mafunzo ya kuokoa wagonjwa mahututi yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Happy
Mabonka akifanya mazoezi kwa vitendo ya kuokoa maisha ya mgonjwa mahututi
wakati wa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa wauguzi walioajiriwa hivi karibuni
jijini Dar es Salaam.
Picha na: Khamis Mussa
*****************************************************************************************************************
Wafanyakazi wapya Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa
mahututi na wagonjwa wa dharura wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkuu wa timu ya kuratibu
jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi na wadharura kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Faraji Lydenge alisema mafunzo hayo yatawasaidia
wauguzi hao kuupampu moyo wa mgonjwa uliosimama ili kusaidia damu kwenda kwenye
moyo na sehemu nyingine za mwili.
Dkt. Faraji ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha huduma ya dawa
za Usingizi kwa wagonjwa wa moyo alisema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa
wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi JKCI ili kuifanya taasisi hiyo kuwa kituo
cha ubora katika kuhudumia wagonjwa hivyo wakaona kuna umuhimu pia wa kutoa
mafunzo hayo mapema kwa waajiriwa hao ambao wameripoti kazini wiki tatu
zilizopita.
“Moyo ukishindwa kufanya kazi na kusimama huduma ya dharura
isipofanyika ndani ya dakika tano za mwanzo ubongo wa mgonjwa unakosa damu ya
kutosha na hewa ya oksijeni ya kutosha hivyo kuleta athari kwa mgonjwa kwani
ubongo wake unaweza ukafa, ama mgonjwa akapoteza maisha yake”, alisema Dkt.
Faraji.
kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Afisa Muuguzi Samweli
Mpiga alisema waajiriwa wapya katika Taasisi hiyo wameongezewa ufahamu wa kuona
viashiria vya mtu ambaye anakwenda kupoteza fahamu, mapigo ya moyo kusimama na
upumuaji kusimama.
“Tumewafundisha waajiriwa hawa ambao wako katika Idara ya
Uuguzi ili kama watakutana na wagonjwa ambao mioyo yao inaenda kusimama watawasaidia
na kuokoa maisha ya wagonjwa ambao
wanatutegemea”, alisema Samweli.
Samweli ambaye pia ni Muuguzi katika chumba cha wagonjwa wa
dharura na mahututi alisema kupoteza fahamu, mapigo ya moyo kusimama au
upumuaji kusimama humtokea mtu yoyote na wakati wowote sio kwa wagonjwa tu
hivyo ni muhimu mafunzo hayo watu wote wakayafahamu ili wanapokutana na mtu anayehitaji
kupatiwa huduma ya dharura waweze kusaidia na kuokoa maisha yake.
“lengo letu kuu la kufaya mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa
moyo hausimami maana moyo ndio unaosambaza damu kwenye moyo wenyewe na kwenye
ubongo ambavyo hivyo ndivyo viungo vikuu viwili ndani ya mwili havitakiwi
kukosa damu”, alisema Samweli.
Naye Muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Irene
Mallya ambaye amepatiwa mafunzo hayo alisema sehemu anayofanya kazi inahitaji kujua
jinsi ya kutoa huduma ya kuokoa maisha ya mgonjwa hivyo mafunzo hayo
yatamsaidia kufanya majukumu yake vizuri.
“Endapo mgonjwa akipata tatizo la moyo kusimama nitaenda
kutumia mafunzo haya kuokoa maisha yake, ninaomba tuendelee kupewa mafunzo mbalimbali
ambayo yatatusaidia katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaohitaji huduma
zetu”,
“Wauguzi wenzangu tunapopata nafasi ya kujifunza tutumie
nafasi hiyo vizuri kwani vitu huwa vinabadilika, tuwe wepesi kutafuta mbinu
mpya kuboresha huduma zetu na kuokoa maisha”, alisema Irene.
Comments
Post a Comment