Dkt. Kisenge aongoza jopo la wataalamu kutibu moyo Arusha

 

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda akizungumza na wananchi waliofika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali katika kambi ya matibabu ya siku saba inayofanyika bila malipo yoyote yale. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye taasisi yake inashiriki katika kambi hiyo  kwa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi taarifa ya upimaji wa moyo aliomfanyia Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Arusha Shabaan bin Juma wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku saba ya magonjwa mbalimbali inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na madaktari wa KilMed Air ambao wanatoa huduma ya matibabu ya dharura katika maeneo yasiyofikika kirahisi ikiwemo kwa watalii wanaopata changamoto za kiafya wakati wanapanda mlima Kilimanjaro na wanapotembelea hifadhi za taifa kanda ya Kaskazini. Dkt. Kisenge alikutana na madaktari hao wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku saba ya magonjwa mbalimbali inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

**************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika bila malipo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

Wataalamu wa Taasisi hiyo wakiogozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wanatoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima.

Dkt.Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema wameamua kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo hivyo basi aliwaomba wananchi wa mkoa wa Arusha pamoja na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

“Huduma hii inatolewa bila malipo yoyote yale, ninawaomba wananchi watumie nafasi hii kupima afya zao ili wajue kama wanamatatizo na kuanza matibabu mapema na wale ambao hawatakutwa na matatizo wajue jinsi ya kujikinga kwani gharama ya kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo ni kubwa”.

“Katika kambi hii tunatoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo pamoja na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo, wale tunaowakuta na matatizo tunawapa dawa za kutumia na ambao tunawakuta na matatizo yanayohitaji uchunguzi zaidi tunawapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge.

Akizungumza na wananchi wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paulo Makonda aliwashukuru wakuu wa hospitali za umma na binafsi nchini pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na huduma za afya kwa kuitikia wito wa kushiriki kambi hiyo ya wiki moja ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Mhe. Makonda alisema anatambua wapo wananchi wanashindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na ugumu wa maisha na ukubwa wa gharama za matibabu hivyo kambi hiyo itawasaidia wananchi kupata matibabu ya kibingwa bila gharama zozote zile.

 “Serikali zote duniani zimeweka bima ya afya ili kuwasaidia wananchi kupata huduma za matibabu hata pale watakapokuwa hawana fedha za kulipia huduma hizo, ninawaomba tumieni vipato mlivyonavyo ili muweze kujiunga na bima za afya  zitakazowawezesha kupata huduma ya matibabu pindi mtakapoumwa”, alisema Mhe.Paul Makonda.

Alisema wagonjwa watakaozidiwa kwenye zoezi hilo watabebwa kwa Helkopta na  kupelekwa hospitali mbalimbali ikiwemo mount Meru kwa matibabu zaidi lengo ni kila mwananchi apate matibabu na apone.

Katika hatua nyingine akitoa salamu zake kwa njia ya simu kwenye kambi hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kutoa msaada kwa mahitaji mengine yatakayohitajika.

Mhe. Rais alimpongeza mkuu wa mkoa wa Arusha kwa kuandaa kambi hiyo ambayo imelenga kuwapatia matibabu wananchi wenye magonjwa mbalimbali na kusema kuwa anatambua kuwa kuna wananchi wengine wanashindwa kupata matibabu kutokana na gharama kubwa hivyo wachangamkie kambi hiyo.

Kambi hiyo ya siku saba ya matibabu inatibu magonjwa mbalimbali ikiwemo moyo, afya ya akili, figo, koo, kinywa, masikio, kufua kikuu, magonjwa ya akina mama, nimonia, mifupa, tumbo.

Zoezi hilo linashirikisha wafanyakazi wa afya 450 wakiwemo madaktari bingwa na madaktari wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara na vipimo mbalimbali.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari