Wahandisi wafanyiwa uchunguzi wa viashiria vya magonjwa ya moyo






Mtaalamu kutoka kampuni ya Sakaar Healthtech Limited Alfred Moshi akiwaelezea wahandisi namna kifaa maaluumu kijulikanacho kwa jina la DOZEE kinachotumika kufuatilia maendeleo ya mgonjwa anayetibiwa akiwa nyumbani kinavyofanya kazi wakati wa mkutano wa 30 wa wahandisi washauri uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) jijini Dar es Salaam


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Faizat Ndosa akimpima shinikizo la damu mhandisi kutoka nchini Nigeria aliyetembelea banda la JKCI wakati wa mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Africa) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Wahandisi walioshiriki mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Afrika) wakiwa katika foleni ya kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwenye banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu wa huduma za afya mtandao kutoka kampuni ya Cloudscript inayofanya kazi na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Beatrice Mmari akiwafundisha wahandisi namna ya kutumia huduma ya afya mtandao kupitia mfumo wa Cloudscript walipotembelea banda la JKCI wakati wa mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Africa) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli George akimpatia ushauri muhandisi aliyepatiwa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Africa) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Picha na: JKCI

*******************************************************************************************************************

Wahandisi kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuijali jamii na kuwapelekea huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na wahandisi waliotembelea banda la JKCI lililokuwa katika maonesho yaliyofanyika wakati wa mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Africa) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo Mhandisi Raphael Joseph alisema JKCI imewathamini wahandisi kwa kuwafikishia huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo huduma ambayo wameipata kirahisi.

“Huduma mnayoitoa hapa leo mmetuokoa sisi wahandisi lakini sio sisi tu bali mmeokoa kundi kubwa la watu wanaotuzunguka kwani tunapopata changamoto za kiafya familia zetu zinakuwa kwenye changamoto pia”, alisema Raphael

Raphael alisema nimuhimu vikao mbalimbali vya kisekta na vya serikali wataalamu wa afya wakahusishwa upande wa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kuwasaidia kujitambua.

Kwa upande wake mhandisi Benard Malongo alisema mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika umewatendea haki washiriki kwa kuwafikishia huduma za uchunguzi wa afya.

Benard alisema watu wanapopewa nafasi ya kuchunguza afya zao watumie nafasi hizo vizuri kwani huduma za matibabu ni za gharama na wananchi wengi mara nyingi hushindwa kumudu gharama hizo.

Akielezea mwitikio wa kupima afya kwa wahandisi hao Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli George alisema jumla ya wahandisi 96 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kupewa ushauri kuhusu lishe na afya bora.

Dkt. Samweli alisema watu 14 walikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wawili walikuwa na tatizo la sukari iliyo juu sana matatizo yaliyohitaji kufanya uchunguzi zaidi hivyo kupewa rufaa kufika JKCI ili waweze kufanyiwa vipimo vikubwa zaidi.

“Mbali na shinikizo la juu la damu wapo tuliowakuta na tatizo la sukari kuwa juu sana ambapo mtu mmoja tumemkuta kiwango cha sukari yake kwenye damu kuwa 33 ambayo inaweza kumsababishia kupoteza maisha”, alisema Dkt. Samweli

Wahandisi waliotembelea banda la JKCI wametoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Tanzania, Zambia, Nigeria na Uganda.



Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari