RC Makonda: Changamkieni fursa ya kutibiwa moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda maendeleo ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wanaotibiwa katika banda hilo wakati wa kambi maalumu ya kupima magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo huduma inayotolewa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge akisalimiana na mkazi wa Arusha aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya kupima magonjwa mbalimbali inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evelyne Furumbe akimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa kambi ya maalumu ya matibabu ya siku saba ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.
*************************************************************************************************************************************************************************************
Wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wametakiwa
kuchangamkia fursa ya kupima magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo huduma
inayotolewa bila malipo yoyote yale katika kambi ya matibabu ya siku saba inayofanyika
katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Rai
hiyo imetolewa leo na Mkuu wa mkoa huo Mhe. Paul Makonda wakati akizungumza na
wananchi waliokuwa wanasubiri kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu
ya moyo zinazotolewa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mhe. Makonda alisema wataalamu kutoka JKCI wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt.Peter Kisenge wako katika uwanja huo kwaajili ya kutoa huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Dkt. Kisenge ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na
mishipa ya damu, kumpata daktari huyu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji siyo
jambo rahisi leo hii yupo hapa kwetu amekuja kutuhudumia wananchi tuitumie
nafasi hii vizuri kwa kuja kupima afya za mioyo yetu”, alisema Mhe. Makonda.
Kwa upande wake Dkt. Kisenge alisema tangu waanze upimaji huo
siku ya jana hadi leo wameona zaidi ya wagonjwa 200 na asilimia 45 ya
waliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na kuna ambao
wameshaanza kupata madhara ya ugonjwa huo.
“Tumewapa rufaa wagonjwa 30 hadi sasa ambao watakwenda
kutibiwa katika taasisi yetu kati yao 18 tutawachunguza mishipa ya damu ya moyo
ambayo inaonekana imeziba na kushindwa kupitisha damu vizuri. Wengine wanamatatizo
ya mfumo wa umeme wa moyo na mioyo yao kufanya kazi katika kiwango cha chini”,
alisema Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi huyo mtendaji alisema katika kambi hiyo
wanawashirikiana na wataalamu kutoka hospitali mbalimbali za Arusha ambao
wanawajengea uwezo wa jinsi ya kuwatibu na kuwatambua wagonjwa wa moyo.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma ya matibabu katika
banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walishukuru kwa huduma
waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua hali za afya za mioyo yao.
Francis Noor mkazi wa Arusha aliwaomba wakuu wa mikoa mingine
kuiga mfano wa mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Mkonda ili wafanye kambi za
uchunguzi na matibabu ya magonjwa
mbalimbali ambazo zitawasaidia wananchi wenye vipato vya chini kupata huduma za
kibingwa za matibabu.
“Nimefika hapa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
nimepata huduma za matibabu ya moyo na vipimo ambavyo sikutegemea kuvipata
nimeonana na Dkt. Kisenge amenihudumia vizuri na kunipa ushauri”.
“Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan na mkuu wa mkoa Mhe. Makonda ambao wamefanikisha kupatikana kwa huduma
hii , mimi unavyoniona unaweza kusema nina hela nyingi lakini uchumi wangu ni
wa hali ya chini. Miaka minne iliyopita niliandikiwa kufanya vipimo vya moyo
nikashindwa kutokana na hali ya uchumi lakini leo hii nimeweza kupata huduma
hii”, alishukuru Noor.
“Ninashukuru kwa huduma niliyoipata ninawaomba wananchi wenzangu waje kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambayo inatolewa bila malipo yoyote yale. Ninawashukuru viongozi wetu kwa kutujali sisi wananchi wanyonge wenye kipato cha chini”, alishukuru Etropia Nikolaus.
Comments
Post a Comment