Huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zafika Namtumbo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akielezea namna huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakavyofanyika katika Wilaya ya Namtumbo kuanzia
tarehe 8 hadi 13 mwezi Julai mwaka huu wakati wa mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo na Mkuu wa Divisheni ya
Afya, ustawi wa jamii na huduma za lishe Dkt. Aaron Hyera akielezea hali ya
afya ilivyo kwa wananchi wa Namtumbo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
kuhusu kambi maalumu ya siku sita ya uchuguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo
kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba itakayofanyika katika
Wilaya hiyo kuanzia tarehe 8 hadi 13 mwezi Julai mwaka huu.
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakisikiliza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya
siku sita ya uchuguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan tiba mkoba itakayofanyika katika Wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma kuanzia tarehe 8 hadi 13 mwezi Julai mwaka huu.
Na: JKCI
*************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
ofisi ya Mbunge wa jimbo la Namtumbo Mhe. Vitta Rashidi Kawawa kufanya kambi
maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba.
Kambi hiyo maalumu ya siku sita itakayoanza tarehe 8 hadi 13
Julai mwaka huu inatarajiwa kufanyika kwa siku mbili katika Hospitali ya
Halmashauri ya Wilaya, siku mbili katika Kituo cha afya cha Lusewa na siku
mbili katika Kituo cha afya cha Mputa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mhe. Vitta Rashidi Kawawa alisema ofisi yake
imeamua kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya
moyo pamoja na elimu ya lishe bora ili waweze kuepukana na magonjwa hayo ambayo
yamekuwa tishio katika jamii.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha program ya tiba mkoba
inayotolewa na wataalamu wa JKCI kuwafikia wananchi wasioweza kufuata huduma
hizi mahali zilipo na kuweza kuwapa ujuzi wataalamu waliopo katika Hospitali za
Wilaya na Mikoa”, alisema Mhe. Vitta.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Mbunge wa jimbo la Namtumbo anafunga
wigo wa kuanza kuwafuata wananchi waliopo katika wilaya mbalimbali hapa nchini.
“Mbunge huyu anawajali wananchi wake ndio maana ameweza
kuandaa kambi hii maalumu kuwafikisha wananchi huduma za kibingwa za matibabu
ya magonjwa ya moyo katika kata za Wilaya ya Namtumbo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema katika kambi hiyo wataangalia magonjwa
ya moyo ya watoto, magonjwa ya shinikizo la damu, magonjwa ya valvu za moyo,
matatizo ya mishipa ya damu na magonjwa mengine ya moyo.
“Tunawaomba wananchi wa Wilaya ya Namtumbo kujitokeza kwa
wingi kupima afya zenu hata kama hamna dalili ni vizuri mkatumia fursa hii
kupima na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wetu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema Magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo
magonjwa ya moyo ndio yanayochangia vifo vingi duniani hivyo kama wananchi
wataweza kufuata mfumo bora wa maisha wataweza kuepukana na magonjwa hayo kwani
kinga ni bora zaidi ya tiba.
“Kupitia kambi hii ya matibabu bila gharama kwa wananchi wa
Namtumbo JKCI itaendelea kuwapa ujuzi wataalamu wa Namtumbo na hapo baadaye
tutatengeneza kituo endelevu cha matibabu ya moyo katika Wilaya ya Namtumbo”,
alisema Dkt. Kisenge
Naye Mnganga mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Aaron Hyera alisema
huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zitakazofanyika kwa
wananchi wa Wilaya ya Namtumbo zimegharamiwa na Mbunge wa jimbo la Namtumbo.
“Ama hakika Mhe. Vitta Kawawa anawajali watu wake hasa katika
eneo la afya kwasababu bila afya hakuna maendeleo ukizingatia wananchi wa
Namtumbo wanafanya shughuli za kuzalisha mazao ya kilimo hivyo inahitaji nguvu
na afya njema kwa mafanikio ya Wilaya”, alisema Dkt. Aaron
Dkt. Aaron ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Afya, ustawi wa
jamii na huduma za lishe alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wa Namtumbo
wanaenda kupata nafasi ya kujifunza ili hapo baadaye waweze kuendelea kuwatibu
wale watakahitaji huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
“Huduma hizi zinaenda kuwapunguzia wananchi wa Namtumbo gharama,
adha na usumbufu ambao wangeweza kuupata kusafiri kutoka Namtumbo hadi Dar es
Saalam kwaajili ya kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”, alisema Dkt.
Aaron
Dkt. Aaron aliwashukuru Mbunge wa jimbo la Namtumbo Mhe. Vitta Kawawa na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI kwa ushirikiano walioufanya kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi wa Namtumbo kwani watu wengi wenye magonjwa ya moyo katika Wilaya hiyo ni kuanzia umri wa miaka 40 na kuendelea ambao wengi wao wangeshindwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mahali zilipo.
Comments
Post a Comment