Watu 1,628 watibiwa moyo katika maonesho ya Sabasaba


Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Suleiman Aboud Jumbe akimkabidhi tuzo ya mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma za afya na matumizi ya teknolojia katika tiba Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda jana wakati wa kufunga maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam (Sabasaba).

Baadhi ya washiriki wa maonesho ya sabasaba kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifurahia baada ya kupokea tuzo ya mshindi wa pili kwa utoaji  wa huduma za afya na matumizi ya teknolojia katika tiba wakati wa kufunga maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam.


Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stanley Dickson akitoa elimu ya lishe bora kwa mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma zinazotolewa wakati wa maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam yaliyomalizika jana katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.


Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nicole Kinyawa akimpatia ushauri mara baada ya kupima vipimo vya moyo mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo lililokuwa katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam.


Mhudumu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sikudhani Simbeye akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo lililokuwa katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam yaliyomalizika jana katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

********************************************************************************************************************

Watu 1628 wamepata huduma za ushauri, uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam (Sabasaba).

Aidha watu 435 wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography –ECHO) huku watu 424 wamefanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography –ECG).

Akizungumza wakati wa kuhitimisha maonesho hayo jana jijini Dar es Salaam Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda alisema watu 111 waliokutwa na matatizo mbalimbali ya moyo wamepewa rufaa kufika Taasisi ya Moyo kwaajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

“Katika maonesho haya tumetoa huduma za vipimo katika maabara yetu inayotambulika kimataifa kwa watu 326 kwa kuwapima vipimo mbalimbali vikiwemo vya homa ya ini, utendaji kazi wa figo, utendaji kazi wa ini,mafuta kwenye damu, kiwango cha chumvi kwenye damu, na tezi dume”, alisema Anna

Anna alisema watu 25 walipatiwa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini baada ya watu hao kufanya kipimo cha kuangalia ugonjwa huo na kukutwa wako salama.

Aidha Anna alisema wataalamu wa taasisi hiyo pia walitoa matibabu kwa raia za kigeni 14 ambao walitoka katika nchi za China, Ujerumani, Iran, Marekani, Japan, Malawi, Comoro, Congo na Zambia.

“Maonesho ya Sabasaba ni maonesho yakimataifa ambayo uhusisha watu kutoka nchi mbalimbali ambao baada ya kusikia kuhusu huduma zetu walitumia fursa hiyo ya utalii tiba kufika katika banda letu kipima afya zao”, alisema Anna

Kwa upande wake Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius Birago alisema watu wengi waliofanyiwa vipimo katika banda la JKCI wamekutwa na tatizo la shinikizo la damu ambapo kati yao wapo waliokuwa wakijijua kuwa na tatizo hilo huku wengine kutojua kama wana tatizo la shinikizo la juu la damu.

“Natoa rai kwa watanzania kutumia fursa za upimaji wa afya zao pale zinapokuwa zimewasogelea, wanapotembelea maonesho kama haya wakikutana na huduma za uchunguzi wa afya wasisite kupima afya zao na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu”, alisema Dkt. Birago

Dkt. Birago alisema Huduma za afya zinapofanyika katika maonesho kama ya Sabasaba zinakuwa zimelenga kuwafikia wananchi hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kufuata huduma hizo mahali zilipo.

“Tunaamini wale tuliowapatia rufaa wakati wa maonesho ya Sabasaba wataweza kufika katika taasisi yetu kwaajili ya matibabu zaidi kupunguza athari kubwa zinazoweza kuwatokea kama watachelewa kupata matibabu”, alisema Dkt. Birago

Naye afisa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stanley Dickson alisema watu 800 walipata elimu na ushauri wa lishe bora ambapo kati yao asilimia 80 walikuwa na uzito uliopitiliza ambao kwa namna moja unaweza kuleta madhara katika afya zao.

Stanley alisema katika mahojiano na watu hao imeonyesha watu wengi hawana tabia za kufanya mazoezi hivyo kupelekea kupata uzito mkubwa kutokana na mfumo wa maisha wanaoishi.

“Ili kuepukana na tatizo la uzito mkubwa natoa wito kwa jamii kupunguza matumizi ya vyakula vya wanga hasa wakati wa usiku, kuongeza matumizi ya mboga za majani na matunda na kufanya mazoezi kuiweka miili yatu huru na kuepuka magonjwa yanayoweza kusababishwa na uzito mkubwa”, alisema Stanley.

Katika maonesho hayo taasisi hiyo iliibuka mshindi wa pili katika utoaji wa huduma za afya na matumizi ya teknolojia katika tiba.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024