Wagonjwa 15 kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo iliyoziba kwa asilimia 99
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao
wa Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wakimfanyia mgonjwa upasuaji mgumu
wa kuzibua mishipa ya damu iliyokuwa imeziba kwa asilimia 99 na kushindwa
kupitisha damu vizuri kwa kutumia tundu dogo wakati wa kambi maalumu ya siku
saba inayofanywa na wataalamu hao katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es
Salaam.
Na: JKCI
**************************************************************************************************************
Wagonjwa 15 ambao mishipa yao ya damu ya moyo ilikuwa imeziba
kwa asilimia 99 na kushindwa kupitisha damu vizuri kufanyiwa upasuaj wa moyo kupitia
tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Aidha wagonjwa wengine 10 ambao valvu zao za moyo zilikuwa
zimeziba nao watafanyiwa upasuaji wa kufungua valvu hizo kupitia tundu dogo
lililopo kwenye paja.
Upasuaji hizo zinafanyika katika kambi maalumu ya siku saba inayofanywa
na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kawajika Mwinyipembe
alisema wapo baadhi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo
matibabu yao hayakufanyika hapo awali kutokana na ukosefu wa baadhi ya vifaa.
“Kwakushirikiana na wataalamu kutoka Shirika la Madaktari
Afrika tumeweza kupata vifaa vya kisasa vya matibabu vinavyotumika kuzibua
mishipa ya damu ya moyo iliyoziba kwa asilimia 99 kuwasaidia wagonjwa wetu
lakini pia kuweza kubadilishana uzoefu”, alisema Dkt. Mwinyipembe
Dkt. Mwinyipembe alisema wagonjwa ambao valvu zao za moyo
zimeziba mara nyingi ufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua lakini kutokana na
teknolojia kukua wagonjwa hao siku hizi ufanyiwa upasuaji kupitia tundu dogo.
“Tunatarajia kuzibua vavlu zilizoziba kwa asilimia 99 kwa
wagonjwa 10 bila ya kuwafanya upasuaji wa kufunga kifua, matibabu ambayo
yatamsaidia mgonjwa kupona kwa haraka na kutumia muda mfupi hospitali tofauti
na mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo”, alisema Dkt. Mwinyipembe
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji mdogo wa moyo
kutoka Shirika la Madaktari Afrika Joanna Ghobrial alisema wataalamu kutoka
Shirika la Madaktari Afrika wamekuwa wakishirikiana na wataalamu wa JKCI lengo
likiwa kubadilishana uzoefu na kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya
moyo.
Dkt. Joanna alisema wataalamu wa JKCI wameendelea katika
kutoa huduma za upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali utaalamu ambao huko mbeleni
hawatahitaji wataalamu wa mashirika makubwa kuwasimamia katika kutoa huduma za
upasuaji wa moyo.
“Madaktari Afrika tumekuwa tukishirikiana na Taasisi hii kwa
muda mrefu na matokeo ya ushirikiano wetu tunayaona, hapo baadaye wataalamu wa
JKCI hawatatuitaji tena kwani wameshabobea”, alisema Dkt. Joanna.
Comments
Post a Comment