Ashukuru kwa kusamehewa deni la matibabu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Jushua Kanunga mkazi wa Simanjiro Mkoani
Manyara aliyefika ofisini kwake jana kwa ajili ya kumshukuru kutokana na
Taasisi hiyo kumsamehe Tshs. 5,294,000/= gharama ya matibabu ya mke wake aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo hivi karibuni
Na: JKCI
********************************************************************************************************************
Mkazi wa Simanjiro Mkoani Manyara Joshua Kanunga ameishukuru
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa
wasiokuwa na uwezo.
Shukrani hizo amezitoa wakati akiongea na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipofika ofisini
kwake jana kwaajili ya kumshukuru kutokana na Taasisi hiyo kumsamehe gharama ya
matibabu ya mke wake aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo hivi karibuni.
Kanunga alisema mke wake aliyekuwa na matatizo ya moyo amefanyiwa
upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi hiyo bila malipo kutokana na hali yao ya
kiuchumu kutomudu kulipia gharama za matibabu hayo.
“Naushukuru sana uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kumpokea mke wangu anayesumbuliwa na maradhi ya moyo na kukubali
kumsamehe gharama za matibabu ambazo zilikuwa ni shilingi 5,294,000”, alisema Kanunga
Kanunga alisema mke wake alianza kuumwa tangu mwaka 2017 na
kumtafutia tiba tofauti tofauti hadi ilipofika mwaka 2021 alipompeleka
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na kugundulika kuwa na magonjwa
ya moyo hivyo kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu.
“Namshukuru Mungu mke wangu katibiwa na sasa kaambiwa amepona
tatizo lililokuwa likimsumbua, sasa hivi tunajiandaa kwa ajili ya kuruhusiwa
kurudi nyumbani baada ya kuhangaika kwa miaka sita bila ya mafanikio”, alisema Kanunga
Kanunga aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kubuni mbinu ya kuanzisha Hospitali inayotibu magonjwa ya moyo
hapa nchini ili kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kwenda nje ya nchi
kwa ajili ya kupata matibabu hayo.
“Watanzania wengi hatuna uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa
ajili ya kutafuta tiba, naipongeza sana Serikali kwa kuanzisha Taasisi hii, pia
nawapongeza madaktari waliomhudumia mke wangu kwa upendo bila ya kuangalia
uwezo wetu mdogo wa kiuchumi”, alisema Kanunga
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma
za matibabu kwa wagonjwa wote wenye uwezo wa kulipa na wasio kuwa na uwezo wa
kulipia gharama za matibabu.
“Katika Taasisi yetu tunapokea wagonjwa wanaolipa gharama za
matibabu wao wenyewe, wagonjwa wanaolipiwa na bima za afya, wagonjwa wanaolipia
sehemu ya huduma na sehemu inayobaki Taasisi inawalipia na wagonjwa ambao
hawalipi kabisa huduma za matibabu” alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kuna taratibu za ustawi wa jamii ambazo wagonjwa wasio na uwezo wa
kulipa wanatakiwa kuzifuata na kama watakidhi vigezo Taasisi inawachangia au
kuwalipia gharama za matibabu.
Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi wajiunge na bima za afya ili
ziwasaidie kulipa gharama za matibabu ikiwemo ya moyo kwani matibabu yake ni ya
gharama kubwa.
Comments
Post a Comment