JKCI yapongezwa kwa kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akimsikiliza mtoto anayetaka kuwa daktari bingwa wa moyo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.
Mtaalamu wa vipimo vya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmin Keria akimpima mtoto kipimo cha kuangalia jinsi umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG ) wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo jambo ambalo limesababisha wagonjwa wa moyo kupata matibabu kwa wakati.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Idara ya Tiba Pemba
Massoud Suleiman Abdulla wakati alipotembelea kambi kambi maalum ya siku tano ya
upimaji na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla
Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.
Massoud alisema kambi hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa
wananchi kufanyiwa vipimo na kupata ushauri na wale wanaokutwa na shida wanatibiwa
na wenye shida kubwa zaidi wanapata rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete iliyopo Dar es Salaam.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni rufaa za JKCI kutoka hapa
Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee ni lazima zipitie Hospitali ya Rufaa ya Mnazi
Mmoja iliyopo Unguja lakini uongozi unafanya jitihada ya kuwaombea wagonjwa
waliokutwa na matatizo ya moyo kwenda moja kwa moja kutibiwa JKCI kwa kufanya
hivi kutapunguza mzunguko mrefu wa kupata huduma”, alisema Massoud.
Massoud alisema kuna baadhi ya kambi zilizofanyika changamoto
iliyotokea ni kwa wagonjwa kuchelewa kupata matibabu ya kibingwa lakini
anaamini wagonjwa waliokutwa na matatizo ya moyo watapata matibabu kwawakati
jambo la muhimu ni kwa viongozi kuhakikisha wagonjwa wote waliopewa rufaa
wanakwenda JKCI kutibiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shemu ambaye pia ni daktari bingwa mbobezi
wa magonjwa ya moyo alisema Taasisi hiyo imejipanga kuwafikia wagonjwa wengi wa
moyo kwa kuwafuata mahali walipo ili wapate matibabu kwa wakati.
“Tumekuwa tukikutana na
changamoto ya wagonjwa wetu tunaowatibu kufika JKCI wakiwa wamechelewa
hivyo basi kupitia huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan Outreach Services tunawafuata wananchi mahali walipo na kutoa
huduma za matibabu na vipimo vya moyo”.
“Tunafanya upimaji kwa kushirikiana na wataalmu wenzetu wa
Hospitali za Rufaa, Kanda na mikoa wakati wa upimaji tunawajengea uwezo
wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua wagonjwa wa moyo mapema pamoja na kufanya
vipimo vya moyo kwa kufanya hivyo kumesaidia kwa kiasi kikubwa wagonjwa kupata matibabu
kwa wakati”, alisema Dkt. Shemu.
Dkt. Shemu alisema upimaji huo unaenda sambamba na utoaji wa
elimu kwa wananchi ili waweze kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yakiwemo magonjwa ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha wa kufanya mazoezi,
kula chakula bora, kutokutumia bidhaa aina ya tumbaku, kuepuka uzito
uliopitiliza na kunywa pombe kwa kiasi.
Comments
Post a Comment