Pemba wafikiwa na huduma bobezi za matibabu ya moyo
Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akimwelezea mkazi wa Pemba jinsi upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo jinsi unavyofanyika katika Taasisi hiyo wakati wa kambi ya matibabu ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.
Kiongozi wa timu ya madaktari kutoka Jamhuri ya Serikali ya watu wa China ambao wanafanya kazi Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba Dkt. Jiang Jinhua akizungumza wakati wa kikao cha kuona jinsi ambavyo kambi maalum ya matibabu ya moyo itakavyofanyika katika Hospitali hiyo. Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Abdulla Mzee wanafanya kambi ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa Pemba.
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi hiyo Dkt. Pedro Pallangyo wakati wa kikao cha kuona jinsi ambavyo kambi maalum ya matibabu ya moyo itakavyofanyika katika Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Abdulla Mzee wanafanya kambi ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa kisiwa hicho.
*******************************************************************************************************************************************************************************
Wananchi wa Kisiwa cha Pemba wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima na kutibiwa magonjwa ya moyo katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani Kisiwani humo.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa
ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi ya matibabu ya siku tano
iliyoanza leo katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee.
Dkt. Shemu ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge alisema wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na
wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee wanatoa huduma bobezi za matibabu
ya moyo kwa wananchi na watahakikisha kila anayehitaji kupata huduma hizo
anazipata kwa wakati.
“Tunataka wananchi wote wenye matatizo ya moyo wafikiwe na
huduma bobezi, hivyo basi tumeamua kuwafuata mahali walipo kwani wengine wanashindwa
kuzifuata huduma hizi Dar es Salaam kutokana na changamoto mbalimbali za
maisha”.
“Tumeambatana na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa kutibu na
kufanya vipimo vya moyo, tukimgundua mgonjwa anashida tunamtibu hapahapa na kwa
wale watakaokuwa na matatizo makubwa tutawapa rufaa kuja kutibiwa katika
Taasisi yetu”, alisema Dkt. Shemu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema watu wengi wanaokwenda
Hospitali kupata huduma za matibabu ya moyo wanakuwa tayari wameshapata madhara
ya ugonjwa huo.
Dkt. Pedro alitoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kuepuka
kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo na pale
watakapoona kuna kampeni ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa
mbalimbali wajitokeze kupima afya zao.
“Unaweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kwa kuacha kutumia
bidhaa aina ya tumbaku, unywaji wa pombe uliokithiri, kuepuka kuwa na uzito
uliopitiliza na ili moyo wako uwe na afya njema
fanya mazoezi japo nusu saa kwa siku na kula chakula bora zikiwemo
mbogamboga na matunda”, alishauri Dkt. Pedro.
Kwa upande wake Msaidizi Daktari Dhamana wa Hospitali ya
Rufaa ya Abdulla Mzee Mohammed Faki Salehe alisema wamefurahi kuwapokea wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete ambao watashirikiana nao kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi.
Dkt. Salehe alisema matatizo ya moyo yapo katika ukanda wa
Pwani na katika Hospitali hiyo huduma za matibabu ya moyo zipo lakini hazitoshelezi
kwani wanadaktari mmoja ambaye anakliniki mara mbili kwa wiki kwa siku za
Jumanne na Alhamisi na wagonjwa wanaofikiwa ni wachache.
“Kupitia kambi hii wananchi wengi watafikiwa na huduma za
upimaji na matibabu ya moyo na tumewapokea watu kutoka nje ya Pemba,
ninamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha wananchi wa Kisiwa cha Pemba wanafikiwa
na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.
“Huduma hii inatolewa bila malipo yoyote yale wananchi
wanafanyiwa vipimo vya moyo na wale wanaokutwa na matatizo wanafanyiwa vipimo
vya maabara, X-Ray ya kifua na CT- Scan na kupewa dawa za kwenda kutumia”, Dkt.
Salehe.
Dkt. ZHU Yinjun daktari bingwa wa moyo kutoka Jamhuri ya
Serikali ya watu wa China ambaye anafanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla
Mzee alisema kuwepo kwa kambi hiyo kutamsaidia kubadilishana uzoefu wa kazi na
wagonjwa wengi kutibiwa kwa wakati mmoja.
Nao wananchi waliofanyiwa vipimo na kupata matibabu katika
kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa
imewapunguzia gharama za kwenda Dar es Salaam kufuata huduma ya matibabu.
“Ninashukuru kwa kupata huduma hii hapa Pemba kama
ningesafiri kwenda Dar es Salaam ningetumia gharama kubwa. Nawaomba wananchi
wenzangu muitumie nafasi hii kuja kupimwa na kutibiwa magonjwa ya moyo ”,
alishukuru Rehema Shamte mkazi wa Chakechake.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma
za tiba mkoba zijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata
wananchi mahali walipo ambapo tangu kuanza kwa huduma hii mwishoni mwa mwaka
jana imeshatoa huduma hiyo katika mikoa ya Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Kisiwa
cha Unguja, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Manyara na Pwani.
Comments
Post a Comment