Serikali yatoa shilingi bilioni 3.6 kujenga jengo la utawala na vipimo JKCI
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe akimpa
maelekezo Mhandisi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eng. Haji Mbuta
baada ya kutembelea ujenzi wa jengo la utawala na vipimo la Taasisi hiyo leo
katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Picha na: Khamis Mussa
*******************************************************************************************************
Shilingi bilioni 3.6 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan kujenga jengo la Utawala na vipimo
ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Jengo hilo linalotarajiwa kumalizika mwezi Agosti mwaka huu
linatarajiwa kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku hivyo
kupunguza muda wa kusubiri huduma za vipimo na matibabu ya moyo.
Akizungumza alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Dkt. Seif Shekalaghe alisema kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za
matibabu ya moyo Mhe. Rais alitoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa huduma za
matibabu ya moyo zinaboreshwa hapa nchini
“Jengo moja lililopo kwa sasa linahudumia wagonjwa wa nje,
linatoa huduma za vipimo, kutoa huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kulaza
wagonjwa hivyo kuleta msongamano mkubwa kwa wagonjwa wanaopata huduma JKCI”,
alisema Dkt. Shekalaghe
Dkt. Shekalaghe alisema Wizara inafuatilia hela zinazotolewa
na Mhe. Rais ili ziweze kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa kwa wakati hivyo
kuwataka wakandarasi wa ujenzi huo kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi
uweze kukamilika kwani Mhe. Rais anapenda anapotoa fedha zitumike kama
zilivyopangwa ili aweze kutoa tena fedha nyingine katika kuboresha sekta ya
afya.
“Hadi sasa jengo hili limekamilika kwa asilimia 71, natambua
kwamba ujenzi huu upo nyuma ndani ya mwezi mmoja kwani lilitakiwa kukamilika
mwezi Mei mwaka huu, baada ya ziara ya leo naomba kusiwe na changamoto nyingene
tena kuzuia jengo hilo kukamilika mwezi Agosti”, alisema Dkt. Shekalaghe
Aidha Dkt. Shekalaghe amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI
kuhakikisha kuwa vifaa vinavyohitajika katika jengo hilo vinaandaliwa mapema
ili jengo linapokamilika mwezi wa nane lianze kutumika hapo hapo na kusiwe na
changamoto za kusubiria vitendea kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kumekuwa na uhaba mkubwa wa ofisi
pamoja na vyumba vinavyotoa huduma za vipimo vya moyo hivyo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Taasisi hiyo
mwaka 2021 kwa ajili ya kuzindua mtambo wa Cathlab akawiwa kutoa fedha hizo
lengo likiwa kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema wagonjwa wa moyo wamekuwa wakisubiri kwa
muda mrefu kupata huduma za vipimo vya moyo hivyo kumalizika kwa jengo hilo
kutawapa nafuu wagonjwa kutokusubiri huduma za vipimo hasa upande wa kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO).
“Mitambo itakayowekwa katika jengo la utawala na vipimo vya
moyo itakuwa mikubwa na ambayo inachukua muda mfupi kutoa huduma za vipimo na
majibu ambapo tunatarajia ndani ya masaa mawili mgonjwa anaweza kuwa
ameshafanyiwa vipimo, kupatiwa majibu yake, na kumuona daktari”, alisema Dkt.
Kisenge
Dkt. Kisenge alisema jengo la utawala na vipimo litatoa
huduma za maabara, huduma za vipimo vya ECHO na ECG, eneo maalum kwa ajili ya
wagonjwa wanaotoka nje ya nchi (Medical Tourism), lakini pia kama alivyoshauri
Katibu Mkuu Wizara ya Afya kutakuwa na vyumba vya madaktari kwa ajili ya
kuwaona wagojwa ili kuwapunguzia mzunguko wagonjwa.
Naye Mkandarasi wa jengo hilo kutoka Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) Baraka Killungu alisema jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba
1400 lina ghorofa 4 ambapo kila ghorofa lina ukubwa wa mita za mraba kati ya
290 hadi 330.
Comments
Post a Comment