SACCOS ya JKCI kutoa mkopo wa shilingi milioni 20
Picha na: Khamis Mussa
*******************************************************************************************************************
Mfuko wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ina
uwezo wa kukopesha wanachama wake hadi kiasi cha shilingi milioni ishirini
endapo mwanachama atakidhi vigezo na masharti vilivyowekwa na SACCOS hiyo.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa SACCOS hiyo ambaye ni Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Tulizo shem alipokuwa akizungumza na wanachama
wa SACCOS hiyo hivi karibuni wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Taasisi
hiyo jijini Dar es Salaam.
“Sasa hivi SACCOS yetu inauwezo wa kumpa mwanachama wake
mkopo wa shilingi milioni ishirini endapo mwanachama huyo hisa zake zinauwezo
wa kulipa rejesho la mkopo wake”, alisema Dkt. Shem
Akizungumzia muda wa kupata mkopo Dkt. Shem alisema kwa sasa
mwanachama anaweze kupata mkopo ndani ya muda wa nusu saa endapo kama atakamilisha
maombi ya mkopo kwa wakati.
“Mwanachama wa JKCI SACCOS anaweza kupata mkopo wake ndani ya
dakika thelathini na atalipa marejesho yake ndani ya miezi tisa badala ya miezi
sita kama ilivyokuwa hapo awali, tunafanya hivi ili wanachama wetu waweze
kufanya maendeleo kupitia mikopo wanayochukua”, alisema Dkt Shem.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Idara ya Tiba ya Moyo Dkt. Tatizo Waane
alisema wajumbe wa bodi wa SACCOS ya JKCI wanatakiwa kuangalia fursa mbalimbali
zilizopo katika mazingira ya JKCI na kuzitumia kama chanzo cha kutunisha mfuko
wa chama kwa kuwekeza katika fursa hizo.
“Wajumbe wa bodi ya SACCOS ya JKCI mnaweza kuwekeza katika
usafi na mgahawa huduma zinazotolewa hapa ndani ya JKCI, kama SACCOS itawekeza katika
maeneo haya Taasisi itakuwa inailipa
Saccos na mapato ya SACCOS yataongezeka”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema kwa sasa JKCI baada ya kupewa hospitali ya
Dar Group idadi ya wafanyakazi imeongezeka hivyo ni wakati sasa viongozi wa
SACCOS hiyo kufikisha taarifa kwa wafanyakazi hao ili nao waweze kuwa sehemu ya
Saccos hiyo na kunufaika na mikopo inayotolewa.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwani Novemba mwaka
jana iliikabidhi JKCI hospitali ya Dar Group hivyo wafanyakazi wa Dar group nao
waambiwe umuhimu wa kujiunga na SACCOS hii kuongeza idadi ya wanachama lakini
pia kuikuza SACCOS”, alisema Dkt. Waane.
Naye Meneja wa Benki ya NMB tawi la Muhimbili Frank Makungu alisema
SACCOS ya JKCI ina muda mfupi lakini inamafanikio makubwa hivyo kuwataka
wanachama wa SACCOS hiyo kufuata masharti yaliyowekwa kuifanya SACCOS hiyo
kuendelea kuwa katika ubora wake.
“Nimekuwa nikishauriana na viongozi wa SACCOS hii kuhusu
mambo mbalimbali, leo nawashauri wanachama mkope kwenye SACCOS yenu, mlipe kwa
wakati na muwe mabalozi wazuri wa kuisema vema SACCOS yenu kwa wengine kwani
kwakufanya hivyo SACCOS yenu itakuwa”, alisema Makungu.
Akizungumzia uzoefu alionao katika vyama vya mikopo Afisa
Ushirika Ofisi ya Msajili Msaidizi Olivia Kaiza alisema SACCOS nyingi
zinashindwa kuendelea kwa sababu ya kutegemea posho katika kukata mapato ya Mfuko
hivyo kuitaka JKCI kuhusisha mishahara kulipa mkopo kuliko kutegemea posho.
“Posho ni fedha ya ziada ambayo inaweza kusitishwa wakati
wowote, nawashauri wajumbe wa bodi ya JKCI SACCOS kutotegemea posho kukata riba
za mikopo bali mikopo ikatwe kwenye mishahara maana mshahara ni lazima mtu apate”,
alisema Oliva.
Comments
Post a Comment