Zambia kujifunza upasuaji wa moyo Tanzania
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mwenzao kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wakimfanyia upasuaji wa kuhamisha mshipa wa damu unapeleka damu chafu kwenye moyo na kuuunganisha na mshipa unaopeleka damu hiyo kwenye mapafu moja kwa moja. Daktari huyo yupo JKCI kwa muda wa wiki moja kwaajili ya kujengewa uwezo baada ya kumaliza mafunzo ya upasuaji wa moyo nchini Israel kupitia Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH).
********************************************************************************************************************************************************************
Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia imemtuma
daktari wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili
ya kuongeza ujuzi wa upasuaji wa moyo.
Hospitali hiyo itaanza kutoa huduma za upasuaji wa moyo hivi
karibuni hivyo inaandaa mkakati wa utekelezaji.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizunguma na mwandidhi wa habari
hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema daktari huyo amekuja nchini kujifunza jinsi ya kuanza kutoa huduma ya
upasuaji wa moyo pamoja na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali inayoongozwa
na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema daktari huyo anajifunza vitu vya muhimu vinavyotakiwa kuwepo katika
Hospitali kabla ya kuanza kutolewa kwa huduma ya upasuaji.
“Mwezi wa nne tulisaini mkataba na Hospitali ya Taifa ya Moyo
ya nchini Zambia wa kuwatibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wataalamu wa
afya wa kuwatibu wagonjwa hao”, alisisitiza Dkt. Kisenge.
“Katika kuhakikisha
Hospitali hii inaanza kutoa huduma za upasuaji wa moyo wiki ijayo madaktari wetu
watatu ambao ni wa usingizi, wagonjwa wa dharura na mahututi na upasuaji watakwenda
nchini Zambia kuona ni jinsi gani tutawajengea uwezo katika kutoa huduma za upasuaji
wa moyo ili waanze kutoa huduma hiyo”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema nia ya Taasisi hiyo ni kusaidia nchi
zote za Afrika Mashariki kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kama unaofanywa JKCI na zaidi ili watu wote waweze kupata huduma
bobezi za matibabu ya magonjwa ya moyo inayostahili. Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa
moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema
daktari huyo amekuja kujifunza jinsi atakavyoweza kufanya upasuaji wa moyo
katika nchi yenye rasilimali chache.
Dkt. Godwin alisema amefurahi kukutana na daktari ambaye
ametoka katika mafunzo hivi karibuni nchini Israeli mahali ambapo yeye pia
alipata mafunzo miaka kumi iliyopita na hii imemfanya kukaa naye kwa ukaribu na
kufanya kwa pamoja yale waliyojifunza katika upasuaji mkubwa wa moyo kwa
watoto.
“Ni mara yangu ya kwanza kukutana na daktari huyu tumefanya
kazi pamoja na tumebadilishana mawazo ,pia nimemweleza changamoto tulizokutana
nazo katika kuanzisha upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto na njia ambazo tulitumia kutatua changamoto
hizo ili kujijenga katika upasuji huu wa
moyo”.
“Naamini kwa ushirikiano huu tutawainua na wao kuanzisha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto ili
watoto walioko nchini Zambia wenye matatizo ya moyo wapate matibabu kwa karibu”,
alisema Dkt.Godwin.
Aidha Dkt. Godwin aliushukuru uongozi wa Shirika la Okoa Moyo
wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) lililoko nchini Israel kwa kuwa sehemu
ya kuwajengea uwezo wataalam wa afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka
Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia Ziwa Mudaniso alisema amekuwa na
muda mzuri wa kujifunza kwa madaktari wa
JKCI katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto.
“Nimefika JKCI kwa ajili ya kujifunza namna madakltari hawa
wanavyofanya kazi na ninaahidi kufanya haya pindi nitakaporudi Zambia, kutumia
vifaa tiba vilivyopo kuwahudumia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa
moyo”, alisema Dkt. Ziwa.
Daktari huyo yupo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa muda wa wiki moja kwaajili ya kujengewa uwezo baada ya kumaliza
mafunzo ya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Wolfson iliyopo nchini Israel
kupitia ufadhili ya Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart –
SACH).
Comments
Post a Comment