JKCI – Hospitali ya Dar Group yaboresha huduma za matibabu ya moyo
Mtechnolojia Mionzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Hamisi Athuman akiwaonesha waandishi wa habari moja kati ya mashine mbili za kisasa za kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) zilizofungwa katika Hospitali hiyo. Serikali kupitia JKCI imenunua mashine tatu za kisasa za kupima moyo zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia sita ambazo mbili zimefungwa Hospitali ya JKCI Dar Group na moja itatumika katika huduma za tiba mkoba zinazojulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt.Tulizo Shemu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mashine mbili za kisasa za kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) zilizofungwa katika Hospitali hiyo.
Moja kati ya mashine mbili za kisasa za kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) zilizofungwa katika Hospitali ya JKCI- Dar Group.
**********************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group imefunga mashine mbili za kisasa za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) kwaajili ya kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt.Tulizo Shemu
alisema mashine hizo za kisasa zinauwezo wa kubaini matatizo ya moyo ya
ndani ambayo mtu anayo tofauti na ilivyo kwa mashine zingine.
Dkt.
Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuwepo kwa
mashine hizo katika Hospitali ya JKCI Dar Group kutasaidia watu wengi wa
wilaya ya Temeke na maeneo ya jirani kupata huduma ya matibabu ya moyo
kwa wingi pasipo kutumia muda mrefu.
“Serikali
kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilinunua mashine tatu za kisasa
za kupima moyo zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia sita ambazo mbili
zimefungwa hapa Hospitali ya JKCI Dar Group na moja itatumika katika huduma za
tiba mkoba zinazojulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services ambapo wataalamu wa moyo wanawafuata wananchi mahali walipo na kufanya
matibabu”, alisema Dkt. Shemu.
Dkt.
Shemu alisema tangu Novemba 14 mwaka jana Serikali ilipokabidhi hospitali ya
Dar Group kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) idadi ya wagonjwa
wanaotibiwa magonjwa ya moyo imekuwa ikiongezeka, kwasasa wanaona wagonjwa 30
hadi 40 kwa siku, pia kliniki za moyo ziko kila siku na huduma inatolewa saa 24
ukilinganisha na hapo nyuma ambapo kliniki za moyo zilikuwa
zinatolewa mara mbili kwa wiki siku za Jumanne na Alhamisi.
Alisema
katika Hospitali hiyo pia wanatoa huduma za matibabu kwa magonjwa mengine
tofauti na moyo ambapo huduma zimezidi kuimarika kwa kuongeza idadi ya
madaktari bingwa, kununua vifaa vya kisasa, kuimarisha huduma ya dharura, kutoa
mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wa afya na kuhakikisha dawa zote muhimu
zinapatikana.
Kwa
upande wake Mtechnolojia mionzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Hamisi Athuman alisema mashine hizo zinauwezo wa
kuwapima watoto na watu wazima kwa wakati mmoja, zinauwezo wa kubaini
mtoto aliyepo tumboni kwa mama yake kama ana matatizo ya moyo au la.
“Mashine
hizi zinauwezo mkubwa wa kufanya kazi zinaweza kupima watu hamsini hadi sitini
kwa siku na mbali na kupima moyo zinapima mishipa ya damu kuona kama inapitisha
damu vizuri au la, zinapima mfumo wa tumbo, mkojo na uzazi”, alisema
Hamisi.
Kwa
upande wake Nassoro Tangulu ambaye ni mgonjwa anayetibiwa katika Hospitali ya
JKCI–Dar Group alishukuru uwepo wa hospitali hiyo ambayo imewasaidia kupata
huduma mbalimbali za matibabu yakiwemo ya moyo.
“Mimi
na familia yangu tunatibiwa katika Hospitali hii nilikuwa nakuja hapa kwaajili
ya matibabu ya shingo na mgongo lakini sasa hivi ninatibiwa moyo, ninaamini
uwepo wa mashine hizi utasaidia wananchi wenye matatizo ya moyo na mengine
kupata huduma nzuri na kwa wakati bila kutumia muda mrefu”.
“Nimeanza
kutibiwa katika hospitali hii sasa ni miezi sita hali yangu haikuwa nzuri kwani
sikuweza kwenda kazini kwa muda wa miezi mitatu lakini kwa sasa afya yangu
imeimarika na ninakwenda kazini”, alisema Tangulu.
Tangulu
alitoa wito kwa wananchi wenye magonjwa mbalimbali kwenda kutibiwa katika
Hospitali hiyo kwani kuna wataalamu wa kutosha pia huduma zinazotolewa ni nzuri
na zinapatikana kwa urahisi.
Comments
Post a Comment