Namibia yaipongeza Tanzania kwa kuwekeza katika matibabu ya moyo
Msimamizi wa kliniki maalumu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Afisa Uuguzi Odilia Njau akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia jinsi wanavyowahudumia wagonjwa wanaotibiwa katika kliniki hiyo wakati wabunge hao walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vivienne Mlawi akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia jinsi wanavyowahudumia watoto waliolazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji wanaohitaji uangalizi maalum wakati wabunge hao walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Anjela Muhozya akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia aina ya upasuaji wa moyo unaofanyika katika Taasisi hiyo wakati wabunge hao walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
*************************************************************************************************************************************************************************
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia wameipongeza Serikali kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo jambo ambalo limewafanya watanzania na mataifa mengine kutibiwa moyo hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na wabunge hao leo jijini Dar es
Salaam wakati walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya
kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kujifunza jinsi ambavyo
Tanzania imefanikiwa katika kutoa huduma za matibabu hayo.
Kiongozi wa msafara wa wabunge hao Julieta Kavetuna alisema kufika
kwao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejifunza mambo mengi ikiwa
ni pamoja na kuona mitambo na vifaa tiba
vya kisasa vya kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Nchini Namibia hatuna Taasisi ya Moyo kama hii sisi tuna idara
ya magonjwa ya moyo ambayo iko katika Hospitali ya Taifa, lakini kama Serikali
ikiamua tunaweza kuwa na Hospitali ya moyo inajitegemea ambayo itakuwa inatoa
huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa”.
“Vitu tulivyojifunza hapa ikiwa ni pamoja na kusomesha
wataalamu, kufanya kazi kwa pamoja, kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kununua vifaa tiba vya kisasa tutakwenda kuvifanyia
kazi Namibia, ninaamini miaka michache ijayo nasi tutakuwa na Hospitali ya moyo”,
alisema Julieta.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Anjela Muhozya alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi
hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikiongezeka
hii ni kutokana na kuwa na wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya
kisasa.
Dkt. Angela alisema ili kuongeza ujuzi wataalamu wa Taasisi
hiyo wamekuwa wakifanya kambi maalumu za matibabu na upasuaji wa moyo kwa
kushirikiana washirika wao kutoka mataifa mbalimbali yaliyoko katika Bara la
Ulaya, Marekani, Australia na Asia.
“Tunaishukuru Serikali ambayo imekuwa ikituunga mkono kwa
mambo yote tunayoyafanya kwani imesomesha wataalamu,kutujengea majengo na
kutununulia vifaa tiba nasi kama wataalamu tunahakikisha watu wenye matatizo ya
moyo wanapata huduma bora na kwa wakati”.
“Taasisi yetu inatoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata
wananchi mahali walipo tunatoa huduma hii kwa kushirikiana na wenzetu wa
hospitali husika. Wakati tunatoa huduma hii tunafanya mafunzo ya kuwajengea
uwezo wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwa
kufanya hivi wagonjwa wanatambuliwa mapema na kupata huduma kwa wakati.
Dkt. Angela alisema Taasisi hiyo pia imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi inazopakana nazo mipaka zikiwemo za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudani, Zambia, Congo, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Visiwa vya Comoro.
Comments
Post a Comment